Nasrullah: Marekani inazuia kuangamizwa kikamilifu kundi la kigaidi la Daesh
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i35415-nasrullah_marekani_inazuia_kuangamizwa_kikamilifu_kundi_la_kigaidi_la_daesh
Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa, Marekani inazuia kuangamizwa kikamilifu kundi la kigaidi la Daesh huko Syria na inalisaidia kundi hilo kwa silaha kupitia kituo chake cha jeshi huko Syria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 09, 2017 00:18 UTC
  • Nasrullah: Marekani inazuia kuangamizwa kikamilifu kundi la kigaidi la Daesh

Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa, Marekani inazuia kuangamizwa kikamilifu kundi la kigaidi la Daesh huko Syria na inalisaidia kundi hilo kwa silaha kupitia kituo chake cha jeshi huko Syria.

Sayyid Hassan Nasrullah aliyasema hayo jioni ya jana katika shughuli ya kuwakumbuka makamanda wawili wa Hizbullah waliouawa shahidi wiki iliyopita wakipambana na kundi la Daesh. Amesema kuwa kwa sasa wapiganaji wa kundi la Daesh wako katika sehemu moja ya mji wa Deir al Zour huko Syria na kwamba Marekani inataka kurefesha umri wa kundi hilo. 

Sayyid Nasrullah amesema kuwa Marekani haitaki kuona kundi hilo likiangamizwa kikamilifu na kwamba, jeshi la nchi hiyo linazuia wanajeshi wa Syria na wapiganaji wa Hizbullah kusonga mbele kwenye maeneo yanayodhibitiwa na Daesh huko Syria. 

Magaidi wa kundi la Daesh

Katibu Mkuu wa Hizbullah amesisitiza udharura wa kuangamizwa kabisa kundi la kiwahabi na kitakfiri la Daesh na kusema: Kama saratani hiyo haitaangamizwa kikamilifu itarejea tena katika maeneo iliyokuwa ikiyadhibiti na kufanya mauaji ya kigaidi. Hata hivyo amesisitiza kuwa, njama hizo za Marekani hazitafua dafu na kwamba uhai wa kundi la Daesh unakaribia mwisho.

Kuhusu uhasama wa siku nyingi za Washington dhidi ya Tehran, Sayyid Nasrullah amesema: Tatizo la Marekani na Iran halihusiani na kadhia ya nyuklia bali tatizo ni changamoto kubwa inayotolewa na Iran dhidi ya miradi na mipango ya Marekani na Saudi Arabia katika eneo la Mashariki ya Kati.