Iraq yatangaza rasmi kuangamizwa kundi la kigaidi la ISIS nchini humo
Waziri Mkuu wa Iraq leo ametangaza rasmi kumalizika kwa mafanikio vita dhidi ya kundi la kigaidi la ISIS au Daesh nchini humo.
Akizungumza katika hafla ya kufungua rasmi kongamano la Jumuiya ya Waandishi Habari Wairaqi mjini Baghdad, Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Heidar al Abadi alisema: "Vikosi vya Iraq sasa vinadhibiti kikamilifu mpaka wa Iraq na Syria na hivyo natangza hapa kumalizika vita dhidi ya Daesh nchini Iraq."
Kabla ya hapo, Waziri Mkuu wa Iraq alikuwa ametangaza kuwa baada ya kukombolewa mji wa Rwa wa magharibi mwa mkoa wa Al Anbar, ngome ya mwisho ya ISIS nchini Iraq, umri wa kijeshi wa kundi hilo la kigaidi umemalizika.
Katika hotuba yake, al Abadi ameashiria uamuzi wa hivi karibuni wa rais wa Marekani kuitambua Quds kama mji mkuu wa Israel na kusema: "Hakuna mtu yeyote anayeweza kubadilisha utambulisho wa Quds na Palestina."
Itakumbukwa kuwa Siku ya Jumatano, Trump alikaidi matakwa ya kimataifa na kuitangaza Quds kuwa eti ni mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Watu katika nchi nyingi za Kiislamu wanaendelea na maandamano ya kulaani uamuzi huo wa Marekani.