Mashambulizi ya makombora ya Yemen yaitia kiwewe Saudi Arabia
Viongozi wa serikali ya Riyadh Ijumaa usiku waliitisha kikao cha dharura cha Baraza la Masuala ya Kisiasa na Kiusalama baada ya shambulizi la makombora ya harakati ya Ansarullah lililolenga eneo la Najran huko kusini mwa Saudi Arabia.
Siku hiyo ya Ijumaa harakati hiyo ilivurumusha kombora moja la balestiki la masafa mafupi na kupiga eneo la Najran. Shambulizi hilo liliwatia kiwewe maafisa wa Saudia walioharakia kuitisha kikao cha dharura cha kujadili masuala ya kisiasa na kiusalama na hali ya kieneo na kimataifa. Ripoti zinasema kuwa, kikao hicho cha dharura kiliakisi hali ya kuchanganyikiwa Aal Saud kutokana na vipigo mtawalia vya wanamapambano wa Yemen wanaoongozwa na harakati ya wananchi ya Ansarullah. Harakati hiyo imetangaza kuwa, imejibu uchokozi wa wavamizi wa Kisaudi katika mwaka 2017 kwa kushambulia maeneo mbalimbali ya Saudia na Imarati na vituo vya wanajeshi wao kwa kuvurumisha makombora 45.
Saudi Arabia na washirika wake waliivamia Yemen tangu mwezi Machi mwaka 2015 na hadi sasa nchi hizo zinaendelea kuizingira nchi hiyo kutokea nchi kavu, majini na angani na zimeua maelfu ya raia wasio na hatia na kuwalazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Kuendelea mashambulizi ya Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya watu wa Yemen, njaa na uharibifu mkubwa unaofanywa na wavamizi hao kumeilazimisha harakati ya Ansarullah kujibu mapigo kwa kuvurumisha makombora ya balestiki dhidi ya wavamizi hao. Mashambulizi hayo yanayolenga maeneo muhimu ya Saudia na Imarati yamevuruga kabisa mahesabu ya Riyadh na washirika wake na kuwafanya wachanganyikiwe.
Takriban miaka mitatu iliyopita wakati Wasaudia na waitifaki wao wanaosaidiwa na Marekani na Israel, walipoivamia Yemen na kushambulia maeneo mbalimbali ya nchi hiyo walidhani kwamba watafanikisha malengo yao kwa kipindi kifupi. Hata hivyo muungano huo si tu kwamba haujafikia malengo yake bali sasa mapigano hayo yameondoka katika ardhi ya Yemen na kuingia katika ardhi ya Saudia. Kwa sasa mashambulizi ya makombora ya Ansarullah yanalenga hadi mji mkuu wa nchi hiyo, Riyadh na maeneo ya Imarati hususan kambi na vituo vyao vya kijeshi. Si hayo tu bali vita vya miaka karibu mitatu sasa vya Saudi Arabia dhidi ya watu wa Yemen vinakaribia kuifilisi kikamilifi nchi hiyo kutokana na gharama kubwa za masuala ya kijeshi kwa upande mmoja na vipigo mtawalia vya wanamapambano katika medani za vita.
Kuhusu hali hiyo Mhariri na Mkurugenzi Mkuu wa gazeti la Raiyul Youm linalochapishwa mjini London ameandika katika tahariri ya gazeti hilo kwamba: Tangu miaka elfu tatu iliyopita hadi sasa hakuna jeshi wala utawala wowote wa kifalme ulioweza kuivamia Yemen na kuondoka nchini huko kwa kupata ushindi, na Saudi Arabia pia haitaweza kufua dafu au kupata ushindi nchini Yemen.