Yemen yashambulia kwa kombora kambi ya jeshi la Saudia
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i39265-yemen_yashambulia_kwa_kombora_kambi_ya_jeshi_la_saudia
Vikosi vya jeshi la Yemen vikishirikiana na harakati ya Ansarullah vimeshambulia kambi ya kijeshi ya Saudi Arabia katika eneo la Najran, kwa kombora la balestiki la masafa mafupi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 21, 2018 04:21 UTC
  • Yemen yashambulia kwa kombora kambi ya jeshi la Saudia

Vikosi vya jeshi la Yemen vikishirikiana na harakati ya Ansarullah vimeshambulia kambi ya kijeshi ya Saudi Arabia katika eneo la Najran, kwa kombora la balestiki la masafa mafupi.

Duru za kijeshi zimeiambia kanali ya televisheni ya al-Masirah kuwa, kombora hilo limelenga kambi ya jeshi ya Quwwah iliyoko katika eneo la Najran, yapata kilomita 844 kusini mwa mji mkuu Riyadh.

Hakuna habari yoyote ya maafa wala hasara iliyosababishwa na shambulizi hilo la ulipizaji kisasi la jana Jumamosi wakati wa adhuhuri.

Hata hivyo msemaji wa Jeshi la Saudia amenukuliwa na vyombo vya habari akidai kuwa wamefanikiwa kulitungua kombora hilo la balestiki.

Sehemu ya mashambulio ya anga ya Saudia dhidi ya Yemen

Wiki iliyopita, Jeshi la Yemen liliushambulia kwa kombora uwanja wa ndege wa Jizan, kusini magharibi mwa Saudia ikiwa ni katika hatua ya ulipizaji kisasi kutokana na uvamizi wa Saudia na washirika wake dhidi ya taifa hilo la Kiarabu.

Aidha mwezi uliopita, harakati ya Ansarullah ya Yemen ilifyatua kombora la balestiki kuilenga Kasri ya al-Yamamah, makazi rasmi ya Mfalme Salman wa Saudi Arabia katika mji mkuu Riyadh.