Assad: Syria itaendeleza vita dhidi ya ugaidi kwa msaada wa Iran
Rais Bashar al Assad wa Syria ameashiria mafanikio ya jeshi la nchi iyo katika vita dhidi ya magaidi na kusema: "Watu wa Syria wataendeleza vita dhidi ya ugaidi kwa msaada wa marafiki hasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia"
Rais al-Assad ameyasema hayo Jumamosi mjini Damascus wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Hussein Jaberi Ansari, msaidizi maalumu wa waziri wa mambo ya nje wa Iran katika masuala ya kisiasa. Ansari pia ni mjumbe maalumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mazungumzo ya kutafuta amani Syria yanayofanyika Astana na Sochi.
Katika mkutano huo Rais al-Assad ameongeza kuwa: "Kuendeleza mapambano dhidi ya ugaidi kutaandaa mazingira mazuri ya kutatuliwa kwa amani mgogoro wa Syria."
Iran na Russia zimekuwa zikitoa msaada wa ushauri wa kijeshi kwa serikali ya Syria katika mapambano yake dhidi ya magaidi wanaopata himaya ya baadhi ya nchi za Magharibi na waitifaki wao katika eneo.

Katika kikao hicho cha jana mjini Damascus, Jaberi Ansari alisisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kuiunga mkono Syria hasa katika vita vyake dhidi ya ugaidi.
Bashar al Assad na Jaberi Ansari aidha walijadili kuhusu uhusiano wa kistratijia wa Iran na Syria na azma ya pande mbili ya kuimarisha uhusiano huo katika nyuga mbali mbali hasa vita dhidi ya ugaidi na pia mazungumzo ya ya kitaifa ya Syria katika mji wa Sochi, Russia.
'Kongamano la Mazungumzo ya Kitaifa Syria' limepangwa kufanyika Januari 29-30 huko Socho nchini Russia.