Kuangamizwa DAESH kumetokana na mshikamano wa wananchi wa Syria na Iraq
Mkuu wa Baraza Kuu la Kiislamu la Iraq amesema mshikamano wa wananchi wa nchi hiyo na wenzao wa Syria ndio uliowezesha kuangamizwa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh katika eneo.
Sheikh Hammam Hamoudi ameyasema hayo mjini Baghdad, katika mazungumzo na Mufti Mkuu wa Syria Sheikh Ahmad Badruddin Hasoun.
Mbali na kusisitiza juu ya kuendelezwa harakati ya Waislamu ya kukabiliana na njama chafu za utawala wa Kizayuni, Sheikh Hamoudi amesema, mshikamano na kuwa kitu kimoja wananchi wa Syria na Iraq vimewezesha kupatikana ushindi mkubwa dhidi ya ugaidi.
Mkuu wa Baraza Kuu la Kiislamu la Iraq aidha ametaka zifanyike jitihada kimataifa kuhakikisha wakimbizi wanarejea makwao na kupatikana amani na uthabiti nchini Syria na kuongeza kwamba: kuangushwa ndege ya kivita ya utawala wa Kizayuni wa Israel na jeshi la Syria ni mirathi ya mafanikio liliyopata taifa hilo katika sekta ya ulinzi.
Kwa upande wake, Mufti Mkuu wa Syria Sheikh Ahmad Badruddin Hasoun ameashiria kugonga mwamba njama za utawala wa Kizayuni za kuzusha mifarakano kati ya koo na makabila mbalimbali ya Syria na Iraq na kusisitiza kwamba nguvu na uwezo wa nchi hizo mbili ni nguvu za umma wa Kiarabu na Kiislamu.../