Wahajiri Waafrika huko Israel wafanya maandamano wakitaka kuachiliwa huru wenzao
(last modified Fri, 23 Feb 2018 15:12:21 GMT )
Feb 23, 2018 15:12 UTC
  • Wahajiri Waafrika huko Israel wafanya maandamano wakitaka kuachiliwa huru wenzao

Kufuatia hatua ya utawala haramu wa Kizayuni ya kuwatimua kwa nguvu wahajiri wa Kiafrika katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu zilizopachikwa jina la Israel, mamia ya wahajiri hao wamekuwa wakifanya maandamano mtawalia mjini Tel Aviv kulalamikia hatua ya utawala huo ya kuwaweka jela wahajiri wenzao.

Septemba mwaka jana Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala huo pandikizi akiwa kusini mwa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu alitangaza kwamba, eneo hilo ambalo wanaishi wahajiri hao wa Kiafrika, litaondoka katika udhibiti wa watu hao na kuwarejesha upya walowezi wa Kiyahudi.

Wahajiri hao wakiandamana kwa uchungu

Maandamano ya wahajiri hao wa Kiafrika yaliyoanza jana Alkhamisi ni ya kwanza tangu kuanza kutekelezwa siasa mpya za kuwatimua wahajiri huko katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni. Makumi ya maelfu ya wahajiri wa Kiafrika wengi wao wakiwa ni raia wa Eritrea na Sudan, waliwasili Israel katika miaka ya hivi karibuni kupitia njia ya mipaka ya jangwani kati ya ardhi za Palestina na Misri ambapo walihadaika na kauli za uongo za Wazayuni kwamba eti Israel ni ardhi takatifu iliyoahidiwa. Tayari utawala huo katili wa Kizayuni umetangaza kuwa unawataka wahajiri hao wawe wameondoka hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu na kwamba kinyume na hapo watasukumwa jela kwa nguvu.

Polisi wa Israel wakiwabughudhi wahajiri hao bila huruma

Katika kutekeleza hatua hiyo, polisi wa utawala wa Kizayuni wa Israel hivi karibuni waliwatia jela Waafrika 7 raia wa Eritrea baada ya wakimbizi hao kukataa kupelekwa nchini Rwanda kwa mabavu. Hatua ya kuwaondoa wahajiri hao kwa nguvu na kuwapeleka katika nchi nyingine za kigeni mbali na mataifa yao asili, imekosolewa vikali na makundi mbalimbali ya kutetea haki za binaadamu ndani na nje ya ardhi za Palelistina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.

Tags