Gaidi wa Daesh anayehusika na utegaji mabomu anaswa nchini Iraq
Kituo cha Uchunguzi cha Harakati ya Muqawama wa Kiislamu Nujaba, kimetangaza habari ya kutiwa mbaroni gaidi wa ngazi ya juu katika genge la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) akiwa pamoja na watu wengine watano.
Taarifa iliyotolewa na kituo hicho imesema kuwa, askari wa Iraq wamefanikiwa kumtia mbaroni Abu Yassin, kinara wa utegaji mabomu wa genge hilo la kigaidi linalofuata idolojia ya Uwahabi akiwa na magaidi wengine watano kupitia operesheni iliyofanywa katika mji wa Khanaqin wa jimbo la Diyala linalopakana na Iran.
Kwa mujibu wa habari hiyo, gaidi huyo amehusika na jinai nyingi za utegaji mabomu nchini humo ambazo zimesababisha mauaji ya watu wengi. Wakati huo huo, Yahya al-Zubaidi, msemaji wa kituo cha habari na masuala ya usalama nchini Iraq amesema kuwa, maafisa wa usalama wa nchi hiyo wenye mfungamano na jeshi la polisi katika mkoa wa Nainawa (Nineveh) wamefanikiwa kubaini na kudhibiti maghala ya silaha za kundi hilo la Daesh katika kijiji cha al-Sahj, ambayo ndani yake kumepatikana silaha na zana mbalimbali za kijeshi za genge hilo. Kadhalika maafisa usalama wameweza kunasa mabomu yaliyokuwa yametegwa na magaidi katika mkoa wa al-Anbar magharibi mwa Iraq na kufanikiwa kuyaripua.
Kwa mujibu wa al-Zubaidi, maafisa usalama wa nchi hiyo wamedhibiti pia maguruneti 370 yaliyokuwa ndani ya gari moja lililokuwa linaelekea mjini Baghdad. Licha ya kutangazwa na Waziri Mkuu wa Iraq, Haider al-Abadi kumalizika vita dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh linaloungwa mkono na Marekani, Saudia na mataifa mengine hapo mwezi Novemba mwaka jana, lakini bado kundi hilo limekuwa likifanya hujuma katika maeneo tofauti ya nchi hususan maeneo ya kaskazini ukiwemo mji wa Kirkuk na mashariki mwa mji wa Baghdad.