Jun 06, 2018 14:20 UTC
  • Qatar: Saudia iache kuingiza masuala ya dini katika mgogoro wa kisiasa

Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kiislamu nchini Qatar sambamba na kuelezea mwenendo wa vizuizi vinavyofanywa na Saudia kwa ajili ya kuwazuia raia wa nchi hiyo kuweza kushiriki ibada ya hija, imeitaka Riyadh kuacha kuyaingiza masuala ya kidini katika mgogoro wa kisiasa wa pande mbili.

Taarifa iliyotolewa na wizara hiyo imesema kuwa, tangazo lililotolewa na Saudia kwamba raia wa Qatar watakaoruhusiwa kushiriki ibada ya hija ya mwaka huu watatakiwa kutokea nje ya mipaka ya nchi hiyo kuingia Saudia na kwamba waingie kwa kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Khalid bin Abdulaziz, ni suala lisilokubalika. Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kiislamu nchini Qatar imeongeza kuwa, katika taarifa iliyotolewa na Wizara ya Hija na Umra ya Saudia, hakuna kitu kipya kilichoelezwa kwa ajili ya kutatuliwa vizuizi vilivyowekwa mwezi Juni mwaka jana dhidi ya mahujaji wa nchi hiyo.

Ibada ya Hijja ambayo sasa inatekelezwa na Saudia kama fimbo ya kuziadhibu nchi maadui

Aidha wizara hiyo ya Qatar imeashiria kuendelea vizuizi na hatua za upande mmoja za Saudia dhidi ya raia wa Qatar na kuongeza kwamba, hadi sasa utekelezaji wa ibada ya hija kwa njia ya ardhini bado umefungwa kikamilifu na kwamba hata kuingia uwanja wa ndege wa Jeddah kutokea Doha pia bado kumewekwa vizuizi na sio rahisi kufanya hivyo. Kufuatia hali hiyo, Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kiislamu nchini Qatar imeitaka serikali ya Saudia kuacha kuingiza masuala ya kidini katika mgogoro wa kisiasa kati ya nchi mbili.

Katika masharti mapya ya Saudia dhidi ya Qatar hakuna raia wa nchi wataruhusiwa kuingia Saudia kwa kutoka Qatar moja kwa moja

Hii ni katika hali ambayo miezi kadhaa iliyopita Saudia iliwarejesha kwa kutumia uwanja wa ndege wa Khalid bin Abdulaziz, raia wa Qatar waliokuwa wameingia katika ardhi ya nchi hiyo kwa ajili ya kutekeleza ibada ya umra kwa kutokea Kuweit. Aidha hivi karibuni pia serikali ya Saudi Arabia kupitia Wizara ya Hija na Umra, ilitangaza masharti kadhaa yanayowazuia Waislamu kutoka Qatar kwenda kutekeleza Umra katika mwezi huu wa Ramadhani.

Tags