Russia: IAEA haina ushahidi wowote wa kuitia hatiani Syria
Mwakilishi wa kudumu wa Russia katika Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA amesema kuwa, kutoa madai ya uongo kuhusu Syria kunauondolea itibari wakala huo wa atomiki.
Televisheni ya Russia al Yaum imemnukuu Mikhail Oliyanov, mwakilishi wa kudumu wa Russia katika IAEA akisema jana (Jumatatu) mbele ya Bodi ya Magavana ya wakala huo mjini Vienna Austria kwamba, Syria ni mfano mzuri wa kupambana na silaha za nyuklia na kwamba kutumia ushahidi wa uongo unaotolewa kwa lengo la kuishinikiza nchi hiyo, kunauondolea heshima wakala wa IAEA.
Amesema, madai kuwa Syria inatumia silaha za kemikali kunadhoofisha muundo na heshima ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki na jambo hilo lina matokeo mabaya na ya hatari sana kwa muundo wa Mkataba wa Kuzuia Uenezaji na Uzalishaji wa Silaha za Nyuklia.
Mapigano ya ndani nchini Syria yalianza mwaka 2011 baada ya nchi za Magharibi na vibaraka wao kumimina magenge hatari ya kigaidi nchini humo na kuyasaidia kifedha, kisilaha na mafunzo ya kijeshi.
Kila wakati magaidi hao wanapozidiwa nguvu na jeshi la serikali ya Syria, Marekani na wenzake wanaeneza madai ya uongo kuwa eti Damascus imetumia silaha za kemikali na hufanya mashambulizi ya kivamizi dhidi ya maeneo ya serikali ya nchi hiyo hata kabla ya kuthibitishwa madai yao na bila ya idhini ya Umoja wa Mataifa.
Hii ni katika hali ambayo kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa na serikali ya Barack Obama, rais wa zamani wa Marekani, silaha zote za kemikali ziliondolewa nchini Syria na ikathibitishwa kimataifa kuwa hakuna tena silaha hizo nchini humo.