Dakta Kharrazi: Wamarekani wameitumbukiza Saudi Arabia katika kinamasi
Mkuu wa Baraza la Kistratijia la Uhusiano wa Nje la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Wamarekani wameitumbukiza Saudi Arabia katika kinamasi na hivi sasa Riyadh imegeuka na kuwa mhudumu wao.
Dakta Kamal Kharrazi amesema hayo katika mahojiano yake na mtandao wa habari wa Al-A'had wa Lebanon na kubainisha kwamba, Wamarekani ndio walioitumbukiza Saudia katika kinamasi na kama alivyosema Raid Donald Trump, hivi sasa Washington imeigeuza Riyadh na kuifanya ng'ombe wa kukamuliwa maziwa.
Mkuu wa Baraza la Kistratijia la Uhusiano wa Nje la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amepongeza matunda ya mazungumzo ya Yemen huko Sweden kuhusiana na usitishaji vita na kusema kuwa, Tehran inakaribisha kwa mikono miwili mazungumzo baina ya makundi ya Yemen.
Dakta Kamal Kharrazi amesema kuwa, ana matarajio kwamba, mazungumzo ya Wayemeni yatakuwa na manufaa kwa wananchi wa nchi hiyo masikini ya Kiarabu.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, usitishaji uhasama na mapigano uliofikiwa huko Sweden kati ya makundi ya Yemen ulianza kutekelezwa katika mji wa bandari wa al Hudaydah Yemen alfajiri ya juzi Jumanne kwa wakati wa huko.
Duru ya kwanza ya mazungumzo hayo ilianza Disemba 6 na kumalizika Disemba 13 nchini Sweden. Utawala wa zamani wa Yemen unaoungwa mkono kikamilifu na Saudia ndio uliokuwa upande wa pili katika mazungumzo hayo yaliyofanyika chini ya upatanishi wa Umoja wa Mataifa.