Jeshi katili la Israel lawaua shahidi Wapalestina katika Siku ya Quds
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i53840-jeshi_katili_la_israel_lawaua_shahidi_wapalestina_katika_siku_ya_quds
Kwa akali Wapalestina wawili waliuawa shahidi na jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel jana Ijumaa, wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Quds.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 01, 2019 03:57 UTC
  • Jeshi katili la Israel lawaua shahidi Wapalestina katika Siku ya Quds

Kwa akali Wapalestina wawili waliuawa shahidi na jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel jana Ijumaa, wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Quds.

Shirika la habari la Palestina la WAFA limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, katika tukio la kwanza, kijana wa Kipalestina aliyekuwa na umri wa miaka 16 kwa jina Abdullah Loay Ghaith aliuawa shahidi kwa kupigwa risasi na askari wa Israel, alipokuwa akiingia katika Msikiti wa al-Aqsa mashariki mwa mji mtukufu wa Quds, kwa ajili ya Sala ya Ijumaa.

Habari zaidi zinasema kuwa, askari hao katili wa Israel walikuwa wamekita kambi katika kijiji cha Dar Salah, mashariki mwa Baitulahm (Bethlehem) wakati walipotekeleza ukatili huo. Wizara ya Afya ya Palestina imesema kijana huyo aliaga dunia kutokana na jeraha la risasi iliyompiga kifuani na kupenyeza kwenye moyo wake.

Kijana mwingine wa Kipalestina mwenye umri wa miaka 21 kwa jina Mo'men Abu Tabish, anauguza majeraha ya risasi katika Hospitali ya Beit Jala baada ya kushambuliwa na askari wa Kizayuni karibu na kibla hicho cha kwanza cha Waislamu.

Quds Tukufu inayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni

Katika tukio la pili, kijana mwingine wa Kipalestina ambaye utambulisho wake haujabainika lakini duru za habari zimedokeza kuwa alikuwa na umri wa miaka 19 hivi, aliuawa shahidi baada ya kufyatuliwa risasi na askari polisi wa utawala haramu wa Israel mashariki mwa Quds Tukufu. Polisi ya Israel inadai kuwa kijana huyo alipigwa risasi alipojaribu kumchoma kisu afisa usalama wa utawala huo pandikizi.

Wiki mbili zilizopita, Idara Kuu ya Takwimu ya Palestina ilichapisha ripoti kwa mnasaba wa mwaka wa 71 wa ardhi za Palestina kukaliwa kwa mabavu na utawala bandia wa Israel na kusema: "Idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi katika kipindi cha miaka 71 ni takribani 100,000."