Oct 22, 2019 03:20 UTC
  • Wapalestina waliotiwa mbaroni Saudia wakabiliwa na mateso

Mwanachama wa ngazi ya juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesema kuwa raia wa Palestina waliokamatwa nchini Saudi Arabia wanakabiliwa na mateso mbalimbali.

Samih Abu Zuhri amesema kuwa, Wapalestina ambao wametiwa nguvuni huko Saudia tangu kuanza mwaka huu wa 2019 wanakabiliwa na mateso na kuhojiwa katika mazingira magumu. Abu Zuhri amesisitiza kuwa, baadhi ya Wapalestina waliotiwa mbaroni wamehojiwa na watu kutoka nje ya nchi. Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Hamas ameongeza kuwa, hivi sasa kuna jumla ya Wapalestina 60 waliopo korokoroni nchini Saudi Arabia; baadhi yao wakiwa ni wanachama au waungaji mkono wa harakati ya Hamas. Amesema baadhi ya raia hao wa Palestina wameishi Saudia kwa zaidi ya miaka 30.  

Aidha baadhi ya vyombo vya habari hivi karibuni viliripoti habari ya kutiwa nguvuni nchini Saudi Arabia Abu Ubaydah al Agha mwanachama mwingine wa ngazi ya juu wa Hamas. Abu Ubaydah anashikiliwa mahabusu katika jela ya Dhahban. 

Mwanachama wa Hamas aliyefungwa jela nchini Saudia
 

Kamati ya Taifa ya Ulinzi ya Palestina imewataka vionozi wa Saudi Arabia wawaachie huru wafungwa wa Kipalestina na kuhitimisha siasa hizo za seli za mtu mmoja mmoja za kuwatesea wafungwa nchini humo.

 

Tags