Abubakr al-Baghdadi, kiongozi wa Daesh auawa
(last modified Sun, 27 Oct 2019 07:38:42 GMT )
Oct 27, 2019 07:38 UTC
  • Abubakr al-Baghdadi, kiongozi wa Daesh auawa

Afisa mmoja wa Pentagon nchini Marekani amesema kuwa Abubakr al-Baghdadi, kiongozi wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh ameuawa katika operesheni ya siri iliyotekelezwa kaskazini magharibi mwa Syria.

Jarida la wiki la Marekani la Newsweek limemnukuu afisa huyo wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon, akisema leo Jumapili kwamba al-Baghdadi aliuawa siku ya Jumamosi katika operesheni ya siri iliyotekelezwa na helkopta za jeshi la Marekani katika mji wa Idlib, kaskazini magharibi mwa Syria lakini kwamba uchunguzi zaidi unaendelea kufanywa ili kuthibitisha kifo chake.

Newsweek limesema kuwa katika miaka ya hivi karibuni, al-Baghdadi amelengwa mara kadhaa na operesheni za siri za Marekani lakini amekuwa akinusurika kifo. Kufuatia kusambazwa habari ya kuuawa kiongozi huyo wa magaidi, Rais Donald Trump wa Marekani ameandika kupitia ujumbe wa Twitter kwamba kuna tukio kubwa ambalo limetokea. Rais huyo anatazamiwa kuzungumzia suala hilo baadaye leo Jumapili.

Abubakr al-Baghdadi akizungumza msikitini huko Mosul, Iraq 2014

Mwaka 2014 Abubakr al-Baghdadi alidhihiri hadharani kutoka mafichoni huko katika mji wa Mosul kaskazini mwa Iraq na sauti yake pia ilisikika mara ya mwisho Agosti mwaka huu wa 2019.

Katika miaka ya karibuni, kundi la Daesh linalodhaminiwa kwa hali na mali na Marekani, utawala ghasibu wa Israel na wa Saudi Arabia, liliteka sehemu kubwa ya ardhi za Iraq na Syria na kufanya mauaji na jinai nyingi za kutisha katika nchi hizo.

Kundi hilo pia limetekeleza operesheni nyingi za kigaidi katika nchi za Ulaya, Asia Magharibi na bara la Afrika.