Kutekelezwa makubaliano ya kupunguza mapigano nchini Afghanistan
Makubaliano ya kupunguza mapigano nchini Afghanistan yalianza kutekelezwa Ijumaa iliyopita.
Ijumaa usiku Rais Ashraf Ghani alisema kuwa, makubaliano ya kupunguza mapigano nchini humo kati ya askari wa kigeni, askari wa serikali na kundi la Taleban kwa kipindi cha siku saba, yameanza kutekelezwa. Sambamba na kuashiria suala hilo, Msemaji wa Kundi la Taleban alisema kuwa, tarehe 29 ya mwezi huu Marekani na Taleban watatia saini makubaliano ambayo yatahudhuriwa na waangalizi wa kimataifa. Baada ya wiki kadhaa za mvutano kati ya serikali ya Afghanistan na Marekani juu ya kupunguzwa mapigano na kundi la Taleban nchini humo, hatimaye pande tatu za Washington, Kabul na Taleban, zimekubaliana kutekeleza mpango huo wa wiki moja. Hatua ya serikali ya Kabul ya kukubali mpango wa kupunguza mapigano nchini humo, imekuja baada ya Rais Ashraf Ghani kuhudhuria mkutano wa Usalama wa mjini Munich, Ujerumani na kufanya mazungumzo pembeni ya jukwaa hilo la usalama la kimataifa na viongozi wa Marekani walioshiriki mkutano huo akiwemo Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya Trump . Kabla ya kushiriki mkutano huo Rais Ashraf Ghani alikuwa amepinga mpango wa kupunguzwa mapigano nchini kwake, huku akisisitiza juu ya usitishaji mapigano wa kudumu na kuhitimishwa vita nchini Afghanistan.
Hivyo kutekelezwa mpango wa kupunguzwa mapigano nchini humo kunaashiria kwamba Marekani imeweza kumkinaisha Ashraf Ghani ili akubali mpango huo. Hata hivyo nchini Afghanistan na katika ngazi ya kisiasa ni mrengo wa rais huyo tu ndio uliokuwa ukipinga mpango wa kupunguzwa mapigano, kwani Abdullah Abdullah, Mkuu wa Baraza la Utekelezaji la Serikali ya Umoja wa Kitaifa la nchi hiyo na viongozi wengine wa serikali ya umoja wa kitaifa na kadhalika idadi kadhaa ya viongozi wa vyama na makundi ya kisiasa walikaribisha mpango huo. Shakhsia hao wa kisiasa waliutaja mpango huo kuwa ni uwanja kwa ajili ya kufikiwa makubaliano ya usitishaji wa kudumu wa mapigano, na kuhitimishwa vita na ghasia ndani ya nchi hiyo. Inafaa kuashiria kuwa, madhumuni ya kupunguza machafuko na mapigano nchini Afghanistan ambayo yameungwa mkono na kundi la Taleban, serikali ya Kabul na Marekani ni kustisha vita kwa muda, lakini kwa kuwa kundi la Taleban halikupendezwa na msamiati huo wa 'usitishaji vita' ndipo ikaamuliwa uitwe upunguzaji machafuko nchini humo. Ijapokuwa makubaliano hayo yalipangwa kutekelezwa kwa muda wa wiki moja, lakini baadhi ya vyombo vya habari vinaripoti kuvunjwa makubaliano hayo katika baadhi ya maeneo.
Viongozi wa jimbo la Balkh wametangaza kwamba saa chache baada ya kutangazwa utekelezwaji wa mpango wa kupunguzwa mapigano na machafuko nchini humo, wanamgambo wa Taleban walitekeleza shambulizi dhidi ya ofisi za jimbo hilo. Moja ya changamoto kubwa za ufanikishaji wa mpango huo wa kupunguzwa mapigano nchini Afghanistan, ni kuwepo migawanyiko miongoni mwa kundi la Taleban ambapo hata inakisiwa kuwa huwenda ikahatarisha makubaliano tarajiwa ya amani kati ya kundi hilo na serikali ya Marekani na ya Afghanistan. Kuhusiana na suala hilo Sayyed Intezar Khadem, mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa Afghanistan anasema: "Serikali ya Pakistan inaweza kuwa na nafasi muhimu ya kutekelezwa mapatano ya mpango wa kupunguzwa mapigano nchini Afghanistan." Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na wasi wasi kwamba iwapo mapatano tarajiwa ya amani yatafikiwa kati ya kundi la Taleban na pande nyingine, hatua ya wanachama waliojitenga na kundi hilo ya kutofungamana na mapatano hayo, itairejesha Afghanistan kwenye mapigano na vita.