Muhula wa kupunguzwa mapigano Afghanistan wamalizika kwa kuuawa, kujeruhiwa watu 80
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i59470-muhula_wa_kupunguzwa_mapigano_afghanistan_wamalizika_kwa_kuuawa_kujeruhiwa_watu_80
Takwimu rasmi zilizotangazwa na serikali ya Afghanistan zinasema kuwa muhula wa siku saba wa kupunguzwa mapigano nchini humo, umemalizika kwa kuuliwa na kujeruhiwa watu 80.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 29, 2020 23:07 UTC
  • Muhula wa kupunguzwa mapigano Afghanistan wamalizika kwa kuuawa, kujeruhiwa watu 80

Takwimu rasmi zilizotangazwa na serikali ya Afghanistan zinasema kuwa muhula wa siku saba wa kupunguzwa mapigano nchini humo, umemalizika kwa kuuliwa na kujeruhiwa watu 80.

Kwa mujibu wa takwimu rasmi ya serikali ya nchi hiyo, muhula huo wa siku saba wa kupunguzwa mapigano ulimalizika asubuhi ya Ijumaa ambapo katika kipindi hicho watu 30 waliuawa na wengine 50 kujeruhiwa. Ripoti hiyo imeongeza kuwa askari 21 na raia mmoja ni miongoni mwa watu waliouawa katika majimbo 12 ya Afghanistan ikiwemo Kabul, ambao ni mji mkuu wa nchi hiyo. Mpango wa kupunguzwa mapigano nchini humo ulianza baada ya Marekani na kundi la Taleban kukubaliana kutenga wiki moja kwa ajili ya jambo hilo ambapo pande mbili zilikubaliana kupunguza kiwango cha mapigano. Hayo yanajiri katika hali ambayo awali kundi la Taleban lilikuwa limetoa amri ya kusitishwa aina yoyote ya mashambulizi katika maeneo tofauti ya Afghanistan. Zabiullah Mujahid, Msemaji wa kundi hilo alitangaza Jumamosi ya jana kwamba Taleban imesimamisha mashambulizi yake nchini Afghanistan katika fremu ya kutiwa saini makubaliano na wanadiplomasia wa Marekani kwa lengo la kufikiwa amani nchini humo.

Mazungumzo kati ya kundi la Taleban na Marekani

Amedai kwamba amri hiyo ya usitishaji mapigano imeleta furaha kwa raia wa Afghanistan na kusisitiza kuwa sehemu muhimu katika makubaliano hayo ni upande wa Marekani kutakiwa kutekeleza ahadi zake. Wakati huo huo Rais Ashraf Ghani Ahmadzai wa Afghanistan amesema kuwa serikali ya Kabul haitotiliana saini mapatano ya amani na makundi ya kigaidi likiwemo genge la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) na kwamba kundi la Taleban linatakiwa kujitenga na misimamo yake. Jumamosi ya jana Marekani na Taleban zilikuwa zimepanga kutiliana saini mapatano ya amani mjini Doha, Qatar. Ni muhimu kuashiria kwamba mazungumzo ya pande hizo hayajawahi kuwa na maslahi yoyote kwa raia wa Afghanistan, bali Wamarekani wamekuwa wakitenda jinai mbalimbali kwa kisingizio eti cha kupambana na ugaidi nchini humo.