Jinai za Aal Saudi dhidi ya sekta ya elimu nchini Yemen
Moja ya sekta ambazo zimepata pigo kubwa katika vita vya muungano vamizi wa Saudia dhidi ya Yemen ni sekta ya elimu katika nchi hiyo masikini zaidi ya Kiarabu katika eneo la Asia Magharibi.
Vita vya muungano wa Saudia dhidi ya Yemen vilianza Machi 26 mwaka 2015 na tarehe 26 Machi mwezi uliopita vita hivyo viliingia mwaka wa sita.
Vita hivyo vimesababishia Yemen hasara kubwa ambapo makumi ya maelfu ya watu wamepoteza maisha na miundo msingi karibu yote ya nchi hiyo imeharibiwa.
Kwa mujibu wa ripoti ya Januari 2020 ya Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Watoto (UNICEF), watoto zaidi ya milioni 12 wa Yemen wanahitaji msaada wa kibinadamu na watoto wengine wasiopungua milioni moja ni wakimbizi wa ndani ya nchi.
Kwa mujibu wa Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watoto uliopitishwa Novemba 1989, watu walio chini ya umri wa miaka 18 huhesabiwa kuwa ni watoto. Kwa msingi huo aghalabu ya watoto wanaohitajia msaada wa kibinadamu Yemen au ambao wamelazimika kuwa wakimbizi ni wale ambao wako katika umri wa kuenda shule na huhesabiwa kuwa ni wanafunzi.
Mwaka wa masomo Yemen huanza kila mwaka mwezi Septemba. Katika mwezi wa Septemba mwaka 2019, zaidi ya watoto milioni mbili nchini Yemen hawakupata fursa ya kusoma na vita ndio sababu kuu ya hali hiyo.
Mbali na hayo, idadi kubwa ya watoto Yemen wameuawa, wamejeruhiwa au kufanywa vilema kutokana na vita vinavyoongozwa na Saudia dhidi ya nchi yao. Aidha watoto wengi wa Yemen ni mayatima kutokana na kupoteza mmoja wa wazazi wao katika vita. Kwa msingi huo idadi kubwa ya watoto Yemen wamepoteza fursa za kusoma kutokana na masuala ya kisaikolojia au wamelazimishwa kuacha masomo kwa sababu ya hali ilivyo.
Abdullah An Naimi, mjumbe wa Wizara ya Elimu ya Yemen, akizungumza Jumapili Aprili 5 alisema, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, wanafunzi milioni tano wa Yemen wamekumbwa na matatizo ya kimasomo na kisaikolojia kutokana na hujuma ya muungano wa kivita wa Saudia dhidi ya nchi hiyo.
Hii ni katika hali ambayo, kwa mujibu wa vipengee vya Hati ya Haki za Watoto iliyopitiswa Novemba 1989, haki ya masomo ni moja ya haki muhimu zaidi za mtoto na ni haki ambayo katu haipasi kukiukwa.
Mbali na hayo, watu wenye umri zaidi ya miaka 18 na ni wanafunzi wa vyuo vikuu ni miongoni mwa walioathiriwa vibaya na hujuma ya Saudia dhidi ya Yemen kwani wameshindwa kuendeleza elimu yao ya juu.
Halikadhalika walimu na wahadhiri wa vyuo vikuu ni kati ya kundi la wafanyakazi wa sekta ya elimu ambao wameathiriwa vibaya na vita vya Saudia dhidi ya Yemen na hivyo wameshindwa kufanya kazi zao au wanafanya kazi katika mazingira magumu sana.
Katika ripoti yake ya Januari mwaka 2020, UNCEF ilitangaza kuwa, kutokana na vita na mzingiro wa pande zote dhidi ya Yemen ambao umewekwa na muungano wa Saudia, walimu katika mikoa 11 ya Yemen hawajaweza kupata mishahara yao.
Hali hii imepelekea walimu kuacha kazi zao hizo rasmi na kujishughulisha na harakati zingine za kujipatia pato ambazo haziendani na hadhi yao katika jamii.
Matokeo mengine ya vita vya muungano wa Saudia dhidi ya Yemen ni kuharibiwa shule na vituo vya elimu vya nchi hiyo.
Abdullah An Naimi, mjumbe wa Wizara ya Elimu nchini Yemen anafafanua kuhusu nukta hii na kusema kuwa, zaidi ya vituo au shule 3,500 zimeharibiwa katika hujuma ya Saudia nchini Yemen. Aidha vituo vya kielimu 402 vimeharibiwa au kuteketezwa kabisa katika hujuma hiyo ya Saudia. Hali kadhalika anasema hivi sasa vituo 993 vya kielimu ni makao ya wakimbizi wa ndani ya nchi.
Nao wanafunzi wa Yemen ambao wanapata fursa ya kusoma katika mazingira magumu wanashindwa kupata kalamu na vitabu kutokana na mzingiro wa Saudia dhidi ya nchi yao.
Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa, vita vya muungano wa Saudia dhidi ya Yemen ni chanzo cha hasara kubwa ya kibinadamu wanayopata wanafunzi, wanachuo, walimu na wahadhiri wa vyuo vikuu. Aidha vita hivyo vya Saudia dhidi ya Yemen vimesababisha hasara kubwa ya miundo msingi ambapo shule, vituo vya kielimu na vyuo vikuu vimeharibiwa vibaya sana. Tatizo jingine kubwa ambalo limesababishwa na hujuma ya Saudia dhidi ya Yemen ni ukosefu wa vifaa na shuhula za kielimu.
Nukta ya mwisho hapa ni kuwa, ingawa vita husababisha hasara na madhara makubwa katika sekta zote, lakini hasara katika sekta ya elimu huwa mbaya zaidi kwani huathiri mustakabali wa nchi iliyo vitani, hasa nchi kama Yemen ambayo hata kabla ya vita ilikuwa dhaifu.