Usitishaji vita wa uongo, Saudia yaendeleza mashambulizi Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i60300-usitishaji_vita_wa_uongo_saudia_yaendeleza_mashambulizi_yemen
Msemaji wa Majeshi ya Yemen jana usiku alisema kuwa, muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia unaendelea kufanya mashambulio katika maeneo mbalimbali ya Yemen licha ya kudai kuwa umesitisha mashambulizi.
(last modified 2026-09-14T11:15:43+00:00 )
Apr 11, 2020 02:17 UTC
  • Usitishaji vita wa uongo, Saudia yaendeleza mashambulizi Yemen

Msemaji wa Majeshi ya Yemen jana usiku alisema kuwa, muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia unaendelea kufanya mashambulio katika maeneo mbalimbali ya Yemen licha ya kudai kuwa umesitisha mashambulizi.

Shirika la habari la FARS limemnukuu Brigedia Jenerali  Yahya Saree akikanusha madai ya Saudia ya kusimamisha vita nchini Yemen na kuongeza kuwa, muungano huo vamizi jana Ijumaa ulishambulia mikoa mitatu ya al Baydhaa, Ma'rib na Taiz nchini Yemen ingawa yalikumbwa na upinzani mkali kutoka kwa majeshi ya nchi hiyo.

Msemaji huyo wa vikosi vya ulinzi vya Yemen ameongeza kwamba, wavamizi wa Yemen wamekuwa wakifanya juhudi mbalimbali za kupata turufu ya kuwasaidia katika matukio ya Yemen lakini mara zote wamekuwa wakipata hasara za roho na vifaa vya kijeshi na hivi sasa wamekwama kwenye kinamasi na wameshapata hasara kubwa katika uvamizi wao nchini Yemen.

Jinai za Saudia nchini Yemen

 

Brigedia Jenerali Yahya Saree ameongeza kuwa, siku ya Alkhamisi pia ndege za kivita za muungano vamizi wa Saudia zilifanya mashambulizi nchini Yemen kwa kushambulia maeneo ya mkoa wa al Jawf.

Kabla ya hapo viongozi mbalimbali wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen walikuwa wamelibeza tangazo la kusitisha vita la muungano wa kijeshi wa Saudia na kulitaja kuwa ni “mchezo mpya wa kisiasa wa Saudia na washirika wake.”

Uvamizi wa kikatili wa Saudi Arabia na wavamizi wenzake hasa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) katika nchi maskini ya Yemen umesababisha maafa makubwa ya roho na mali na kuangamiza kila kitu katika nchi hiyo ya Kiarabu.