Kuendelea mashambulizi ya jeshi la Uturuki katika ardhi za Syria
Katika hali ambayo serikali ya Uturuki inawalazimisha raia wake kukaa karantini majumbani, jeshi la nchi hiyo na vibaraka wake, sambamba na kuzivamia ardhi za kaskazini na mashariki mwa Syria limewasababishia hasara kubwa raia wa nchi hiyo ikiwa ni pamoja na kubomoa nyumba zao.
Katika uwanja huo, kumeripotiwa habari mpya zinazoeleza kuwa jeshi vamizi la Uturuki na vibaraka wake, limevishambulia kwa mabomu na mizinga vijiji vya kaskazini mashariki mwa Syria. Askari hao wa Uturuki na vibaraka wake limetumia silaha nzito za mizinga dhidi ya vijiji vya miji ya Tall Tamr na Tall Abū Rāsīn katika mkoa wa Al-Hasakah, kaskazini mashariki mwa Syria. Kiasi kwamba operesheni hiyo imesababisha hasara kubwa kwenye mali za wananchi wa maeneo hayo. Uvamizi wa jeshi la Uturuki katika ardhi za nchi hiyo jirani, umekabiliwa na upinzani mkali wa raia wa Syria, serikali ya Damascus na pia jamii ya kimataifa. Hii ni katika hali ambayo, akthari ya raia wa Uturuki na viongozi wa vyama vya upinzani dhidi ya serikali ya Rais Recep Tayyip Erdoğan pia wamekuwa na msimamo kama huo wakilaani siasa za uvamizi za serikali ya Ankara. Licha ya malalamiko hayo, viongozi wa serikali ya Uturuki hawajakomesha mwendelezo wa operesheni za askari wa nchi hiyo huko kaskazini mashariki mwa Syria. Hii ni katika hali ambayo jeshi la serikali ya Damascus kuanzia miezi kadhaa iliyopita limekuwa likitekeleza operesheni za kuusafisha mkoa wa Idlib kutokana na uwepo wa magaidi. Hata hivyo inaonekana kuwa serikali ya Uturuki na kwa lengo la kuwaunga mkono magaidi na kutafuta njia ya kuwaokoa, imetangaza kupinga vikali aina yoyote ya operesheni za jeshi la Syria katika mkoa wa Idlib.
Hatua ya uingiliaji ya serikali ya Ankara katika masuala ya ndani ya Syria, inajiri katika hali ambayo mwenendo huo unakinzana na misingi na sheria zote za kimataifa. Kuhusiana na suala hilo Haysam Hassoun, kamanda mstaafu wa jeshi la Syria na mtaalamu wa masuala ya kijeshi nchini humo, ameitaja hatua ya Uturuki dhidi ya Syria kuwa ni uvamizi na ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa kwa kusema: "Kiukweli katika uvamizi huu, rais wa Uturuki anahesabika kuwa muhusika mkuu. Kutokana na uungaji mkono wa Rais Recep Tayyip Erdoğan kwa kundi la kigaidi la Jab'hatu Nusra na makundi mengine ya kigaidi, kwa hakika yeye ni sehemu muhimu ya uvamizi wa ardhi ya Syria, na katika hatua ya sasa ameingia katika vita vya moja kwa moja na serikali ya Syria." Mtaalamu huyo wa masuala ya kijeshi amezungumzia pia operesheni za jeshi la Uturuki na kuhusika kwake katika kuikwamisha serikali ya Damascus na raia wa Syria mara kadhaa kwa kusema: "Askari wa Uturuki kwa kushirikiana na makundi ya kigaidi na chini ya uongozi, ulinzi na misaada ya kiintelejensia na ujasusi wao wameingia katika vita nchini Syria na kushiriki katika mashambulizi ambayo yanafanana na yale ya mji wa Saraqib na vitongoji vingine vya Syria."
Ukweli ni kwamba serikali ya Uturuki inafanya njama za kuikwamisha serikali ya Damascus na nchi waitifake wake, ili iweze kufikia malengo yake machafu katika nchi hiyo jirani ya Kiarabu. Ni kwa ajili hiyo ndio maana serikali ya Rais Recep Tayyip Erdoğan ikatangaza upinzani wake kwa operesheni za jeshi la Syria dhidi ya makundi ya ukufurishaji na kigaidi. Askari wa Uturuki wamezivamia baadhi ya ardhi za Syria kwa kisingizio cha kupambana na ugaudi. Hata hivyo baadhi ya duru za habari zimearifu kwamba, askari hao vamizi wa Uturuki sambamba na kutoa mafunzo ya kijeshi na silaha kwa magaidi, wanawachochea magaidi kuendeleza vita dhidi ya serikali halali ya Rais Bashar Al-Assad wa Syria. Ukweli huu haupasi kusahaulika kwamba katika operesheni zote za jeshi la Uturuki ndani ya ardhi ya Syria, idadi kubwa ya raia wa nchi hiyo ya Kiarabu hususan wanawake, watoto na wazee wamepoteza maisha. Kiujumla ni kwamba kwa kuzingatia mashinikizo ya vyombo vya habari na hata serikali za eneo juu ya misaada ya jeshi la Uturuki kwa magaidi, tunaweza kusema kuwa harakati za serikali ya Ankara ndani ya ardhi ya Syria ni zenye lengo tu la kukabiliana na serikali halali ya Rais Assad na kuwaokoa magaidi waliosalia katika nchi hiyo. Hata hivyo serikali ya Erdoğan inapasa kusubiria hatma mbaya kutokana na hatua zake hizo za kichokozi.