Mashambulio ya Saudia yameisababishia sekta ya elimu Yemen hasara ya mabilioni
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i60334-mashambulio_ya_saudia_yameisababishia_sekta_ya_elimu_yemen_hasara_ya_mabilioni
Wizara ya Elimu ya Yemen imesema mashambulio na hujuma zinazofanywa na muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya nchi hiyo maskini ya Kiarabu zimeisababishia sekta ya elimu ya nchi hiyo hasara ya dola bilioni 12.
(last modified 2026-09-14T11:15:43+00:00 )
Apr 12, 2020 23:09 UTC
  • Mashambulio ya Saudia yameisababishia sekta ya elimu Yemen hasara ya mabilioni

Wizara ya Elimu ya Yemen imesema mashambulio na hujuma zinazofanywa na muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya nchi hiyo maskini ya Kiarabu zimeisababishia sekta ya elimu ya nchi hiyo hasara ya dola bilioni 12.

Katika taarifa ya jana Jumapili, wizara hiyo imesema kiwango cha hasara katika sekta ya elimu ya Yemen iliyosababishwa na mashambulio ya kila uchao ya vikosi vamizi kufikia sasa ni riyal trilioni 3 za Yemen sawa na dola bilioni 12 za Marekani.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, shule na vituo vya elimu 412 vimeharibiwa kikamilifu kutokana na hujuma za anga za Saudia dhidi ya taifa hilo maskini.

Wizara ya Elimu ya Yemen imebainisha kuwa, shule 1,491 zimeharibiwa kwa kiasi fulani, huku vituo vya elimu vipatavyo 756 vikifungwa kutokana na mashambulio hayo ya vikosi vamizi vya Saudia na waitifaki wake.

Kadhalika hujuma hizo za Saudia mbali na kuathiri moja kwa moja elimu na muskatabali wa watoto wa Yemen zaidi ya milioni 2, lakini pia zimesababisha watu 196,000 waliokuwa wakifanya katika sekta hiyo kupoteza ajira.

Basi la shule moja Yemen lililoshambuliwa katika hujuma ya anga ya Saudia

Kwa mujibu wa ripoti ya Januari mwaka huu ya Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Watoto (UNICEF), watoto zaidi ya milioni 12 wa Yemen wanahitaji msaada wa kibinadamu na watoto wengine wasiopungua milioni moja ni wakimbizi wa ndani ya nchi.

Mbali na hayo, idadi kubwa ya watoto Yemen wameuawa, wamejeruhiwa au kufanywa vilema kutokana na vita vinavyoongozwa na Saudia dhidi ya nchi hiyo jirani yake, tokea Machi 2015.