Yemen: Tutaendelea kupambana kiume na majeshi vamizi ya Saudi Arabia
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i60438-yemen_tutaendelea_kupambana_kiume_na_majeshi_vamizi_ya_saudi_arabia
Msemaji wa vikosi vya ulinzi vya Yemen amesisitiza kuwa, jeshi la nchi hiyo hiyo likishirikiana na kamati za kujitolea za wananchi litaendelea kusimama kidete mbele ya mashambulio ya majeshi vamizi ya muungano unaoongozwa na Saudi Arabia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 17, 2020 20:12 UTC
  • Yemen: Tutaendelea kupambana kiume na majeshi vamizi ya Saudi Arabia

Msemaji wa vikosi vya ulinzi vya Yemen amesisitiza kuwa, jeshi la nchi hiyo hiyo likishirikiana na kamati za kujitolea za wananchi litaendelea kusimama kidete mbele ya mashambulio ya majeshi vamizi ya muungano unaoongozwa na Saudi Arabia.

Brigedia Jenerali Yahya Saree amesema kuwa, kuumechukuliwa hatua madhubuti na zinazofaa kwa ajili ya kuihami ardhi ya Yemen na wananchi wake mbele ya wavamizi wa Saudia na washirika wao.

Aidha ameeleza kwamba, wananchi wa Yemen katu hawatasilimu amri na watailinda na kuitetea ardhi yao kwa thamani yoyote ile.

Wakati huo huo, ndege za kivita za Saudi Arabia jana  ziliishambulia mikoa ya al Jawf na Maareb huko kaskazini mashariki mwa Yemen. Ndege hizo pia ziliishambulia mara mbili wilaya ya Majzar katika mkoa wa Maareb na kuishambulia mara sita wilaya ya Medghal katika mkoa huo.  

Msemaji wa muungano vamizi huko Yemen unaoongozwa na Saudi Arabia Kanali Turki al Maliki wiki iliyopita alidai kuwa, muungano huo umesitisha vita nchini Yemen.

Hata hivyo Brigedia Jenerali Yahya Saree, Msemaji wa Jeshi la Yemen amesema kuwa, katika muda wa wiki moja iliyopita muungano huo vamizi umetekeleza mashambulio ya anga mara 230 na kufanya mashambulizi 32 ya nchi kavu.

Uvamizi wa kikatili wa Saudi Arabia na wavamizi wenzake hasa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) katika nchi maskini ya Yemen umesababisha maafa makubwa ya roho na mali na kuangamiza kila kitu katika nchi hiyo masikini ya Kiarabu.