Jun 29, 2020 14:25 UTC
  • Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu aitaka Israel iache kupora ardhi za Palestina

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, mpango wa Israel wa kupora ardhi zaidi za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kuziunganisha na ardhi nyingine za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ni kinyume kabisa na sheria.

Michelle Bachelet amesema hayo leo katika taarifa yake maalumu ambapo sambamba na kuukosoa mpango huo wa Israel amewataka viongozi wa Tel Aviv wasitishe mpango wao huo.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ameonya kuwa, kutekelezwa mpango huo kunaweza kuibua machafuko na mapigano yenye maafa zaidi katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Kwa mujibu wa mpango wa kidhalimu wa Marekani wa "Muamala wa Karne" utawala wa Kizayuni umekusudia kuanza kuteka ardhi zaidi za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kuanzia tarehe Mosi mwezi ujao wa Julai 2020 na uporaji huo utayahusu maeneo ya Bonge la Jordan na vitongoji vyote vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi.

Vitongoji haramu vya walowezi wa Kizayuni huko Palestina

Benjamin Netanyahu, kiongozi wa chama cha Likud na Benny Gantz kiongozi wa chama cha Blu na Nyeupe, walifikia makubaliano ya kutwaa asilimia 30 ya eneo la Palestina la Ukingo wa Magharibi na kuliunganisha na ardhi nyingine zilizoghusubiwa za Palestina ifikapo mwezi Julai mwaka huu wa 2020, hatua ambayo imeendelea kukabiliwa na malalamiko ya kila upande.  Uamuzi huo unatathminiwa kuwa ni sehemu ya mpango wa kibaguzi wa Marekani wa Muamala wa Karne.

Makundi ya Palestina na wanaharakati mbalimbali hata wa barabni Ulaya wameendelea kupinga vikali mpango huo wa Israel.

Tags