Jun 14, 2022 07:47 UTC
  • Bachelet kutowania tena Ukamishna wa Haki za Binadamu wa UN

Michelle Bachelet, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ametangaza kuwa hatagombea tena wadhifa huo kwa muhula wa pili.

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari jana, Bi Bachelet alitangaza uamuzi huo kwa kusema: "leo nimeshiriki kikao cha mwisho cha baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa nikiwa Kamishna Mkuu".

Agosti 10, 2018, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilimchagua Michelle Bachelet, rais wa zamani wa Chile kuwa kamishna mkuu wa haki za binadamu wa umoja huo; na kuanzia Septemba mosi mwaka huohuo akashika wadhifa huo uliokuwa ukishikiliwa na Zeid Ra'ad Al Hussein kutoka Jordan.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alieleza kufurahishwa na kuteuliwa kwa Michelle Bachelet kuwa Kamishna Mkuu wa Haki za BInadamu wa UN akimtaja kama "kiongozi wa aina yake wa haki za binadamu kwa ajili ya kipindi kigumu".

Antonio Guterres

Bi Michelle Bachelet alikuwa mwanamke wa mwanzo katika historia ya Chile kushika wadhifa wa urais; na yeye mwenyewe alikuwa mmoja wa waathirika wa ukiukaji wa haki za binadamu. Baba yake Jenerali Alberto Bachelet alikamatwa wakati wa utawala wa dikteta Augusto Pinochet kwa tuhuma za uhaini na kuandamwa na mateso kwa miezi kadhaa. Jenerali Bachelet aliaga dunia hatimaye akiwa kizuizini kutokana na mshtuko wa moyo.

Michelle Bachelet alishika wadhifa wa urais wa Chile kwa vipindi viwili vya kuanzia 2006 hadi 2010 na baadaye 2014 hadi 2018. Aidha kuanzia mwaka 2010 hadi 2013 alikuwa Mkurugenzi wa Shirika la Wanawake la Umoja wa Mataifa.../

 

Tags