Sep 11, 2022 02:25 UTC
  • Kuchaguliwa Kamishna Mkuu mpya wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepasisha kuteuliwa bwana Volker Turk mwanadiplomasia wa Austria mwenye uzoefu wa muda mrefu ndani ya Umoja wa Mataifa kuchukua nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na mtangulizi wake Michelle Bachelet ya Kamishna Mkuu wa umoja huo.

Awali Antonio Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alipendekeza kuwa, Volker Turk achukue nafasi ya Bachelet ambaye muhula wake wa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu ulimalizika tarehe 31 Agosti mwaka huu; ambapo Baraza Kuu la Umoja Mataifa lenye nchi wanachama 193 wa Umoja wa Mataifa Alhamisi iliyopita  liliidhinisha uteuzi huo  kwa kauli moja. Umoja wa Mataifa umesema katika ripoti yake kuwa, Volker Turk ana uzoefu wa siku nyingi na amekuwa mashuhuri katika kuendeleza kazi ya masuala ya haki za binadamu duniani. Taarifa ya Umoja wa Mataifa imebainisha kuwa, moja ya tajiriba kubwa za Volker ni hatua yake ya kuwaunga mkono baadhi ya watu walio katika mazingira hatari duniani, wakiwemo wakimbizi na wale wasio na uraia. Kabla ya uteuzi huo mpya, Volker aliwahi kulifanyia kazi Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) huko Malaysia, Kosovo, Bosnia Herzegovina, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Kuwait. Hata hivyo kuteuliwa Volker Turk kuwa Kamishna mpya wa Haki za Binadamu wa UN kumekabiliwa na ukosoaji mbalimbali.  

Michelle Bachelet, Kamishna Mkuu wa zamani wa Haki za Binadamu wa UN 

Phil Lynch Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Kimataifa wa Haki za Binadamu anasema: Kuteuliwa Turk kushika wadhifa huo hakukuwa wazi na kumefanyika bila ya kushauriana na taasisi za kiraia. 

Kamisheni Kuu ya Haki za Binadamu ni sehemu ya Umoja wa Mataifa ambayo inafanya kazi za kukuza na kulinda haki za binadamu kwa kufuata sheria na kanuni za kimataifa; na uwepo wake pia unachukuliwa kuwa wa lazima katika Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu. Taasisi hiyo iliundwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Disemba 20 mwaka 1993 ili kuendesha mkutano wa kimataifa wa kuunga mkono haki za binadamu. Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu ambaye ni Mkuu wa Kamisheni Kuu ya Haki za Binadamu ndiye anayeratibu shughuli za haki za binadamu za Umoja wa Mataifa, na pia kusimamia kazi za Baraza la Haki za Binadamu la UN katika mji wa Geneva huko Uswisi. Kazi ya Baraza Kuu la Haki za Binadamu ni kusimamia utekelezaji wa vipengee vya mkataba wa haki za binadamu katika nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa.  

Tukichunguza rekodi ya faili la utendaji la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa hasa Baraza la Haki za Binadamu la umoja huo tunashuhudia utendaji unaojumuisha hatua chanya na hasi. Kati ya hatua chanya zilizochukuliwa na baraza hilo chini ya uongozi wa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu ni kulaaniwa mara kadhaa jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi madhlumu wa Palestina na pia kulaaniwa mashambulizi ya Israel dhidi ya Ukanda wa Ghaza. Hasa ikizingatiwa kuwa baraza hilo limetayarisha ripoti ndefu katika uwanja huo baada ya kuchunguza hali ya haki za binadamu katika nchi kama Marekani ambapo ndani ya ripoti hiyo kumeashiriwa kesi mbalimbali za ukiukaji wa haki za binadamu nchini humo; nchi ambayo inadai kuwa na uhuru wa kutosha na mtetezi wa haki za binadamu duniani. Matukio mengi ya ukiukaji wa haki za binadamu nchini Marekani kama ubaguzi mkubwa wa rangi, kukiukwa haki za wafungwa, kukiukwa haki za raia asilia wa nchi hiyo, kukiukwa haki za wanawake, hatua za mabavu dhidi ya wahajiri haramu na wakimbizi na  ukiukwaji mwingine wa haki za binadamu yameashiriwa ndani ya ripoti hiyo; ambapo Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa limetaka kukomeshwa vitendo hivyo tajwa visivyo vya kibinadamu. 

Jinai za Israel dhidi ya Ukanda wa Ghaza 

Pamoja na hayo, Baraza la Haki za Binadamu limedhihirisha katika masuala mengi mengine kwamba linaathiriwa na maslahi ya kisiasa ya nchi zenye ushawishi mkubwa duniani khususan Marekani. Aidha baraza hilo limekuwa likishindwa kutoa jibu kali na linalofaa katika uwanja huo katika baadhi ya masuala ya wazi ya ukiukaji wa haki za binadamu. Mfano wa wazi wa jambo hilo ni jitihada endelevu za nchi za Magharibi za kutaka kulitumia baraza hilo kama wenzo na wakati huo huo kumuweka chini ya mashinikizo Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ili atoe ripoti kuhusu kukiukwa haki za binadamu katika nchi hasimu au zile zinazoipinga Marekani. Marekani ndiyo inayotumia pakubwa suala la haki za binadamu ili kuziwekea mashinikizo nchi nyingine duniani. Mfano wa karibuni wa kadhia hii ni ripoti kuhusu unyanyasaji ulioratibiwa kwa mpangilio maalumu wa China dhidi ya jamii ya  walio wachache katika eneo la Xinjiang. Ripoti hiyo iliyocheleweshwa kwa muda mrefu ilitolewa na Bachelet muda mfupi kabla ya kumalizika muda wake wa kuhudumu katika nafasi ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu. Turk Kamisha Mkuu mpya wa Haki za Binadamu sasa anakabiliwa na kibarua kigumu cha kufuatilia ripoti hiyo tajwa. Dai Bing Naibu Balozi wa China katika Umoja wa Mataifa Alhamisi iliyopita alisema katika kikao cha Baraza Kuu kwamba: China inataraji kuwa Volker Turk atatekeleza majukumu yake kwa kuheshimu kikamilifu haki ya usawa, kutoegemea upande wowote na kujiepusha na masuala ya kisiasa katika utendaji kazi wake.  

Marekani na ukiukaji wa haki za binadamu nchini humo na duniani kwa ujumla 

 

Tags