May 25, 2024 03:41 UTC
  • Rais Samia aungana na viongozi wa mataifa mengine kumuomboleza Ebrahim Raisi

Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameungana na viongozi wa mataifa mengine duniani kumuomboleza Ebrahim Raisi wa Iran.

Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mara nyingine tena ametoa mkono wa pole kwa wananchi wa Iran kutokana na kuondokewa na kiongozi wao Rais Ebrahim Raisi aliyeaga dunia Jumapili iliyopita katika ajali ya helikopta.

Rais Samia Suluhu Hassan jana alikwenda katika ubalozi wa Iran mjini Dar es Salaam na kusaini kitabu cha maombolezo katika ubalozi huo kufuatia Kifo cha Rais wa nchi hiyo Hayati Ebrahim Raisi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisaini kitabu cha maombolezo katika ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Tanzania kufuatia Kifo cha Hayati Ebrahim Raisi 

 

Rais Samia alitumia fursa hiyo pia kumpa pole balozi Hossein Alvandi Bahineh pamoja na maafisa mbalimbali wa ubalozi huo na kueleza kuwa, taifa la Tanzania lipo pamoja na Iran katika kipindi hiki kigumu cha msiba mkubwa.

Helikopta iliyokuwa imembeba Sayyid Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Jumapili jioni Mei 19, 2024 ilipata ajali ilipokuwa ikirejea kutoka kwenye hafla ya ufunguzi wa bwawa la Qiz Qalasi kwenye mpaka wa pamoja wa Iran na Jamhuri ya Azerbaijan.  

Tags