Jun 30, 2021 02:23 UTC
  • UN yataka kung’olewa mizizi ya ubaguzi wa kimfumo duniani

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet Jumatatu wiki hii alitoa wito wa kung'olewa mizizi ya ubaguzi wa kimbari unaofanyika kimfumo dhidi ya watu weusi kote duniani ili dunia isishuhudie tena matukio ya kusikitisha kama lile la muaji ya raia mweusi wa Mrekani, George Floyd.

Michelle Bachelet ambaye amekabidhi ripoti yake yenye kurasa 23 kwa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, amesema hali iliyopo hivi sasa haiwezi kuhalalishwa na kuongeza kuwa: Ubaguzi wa kimbari wa kimfumo unahitajia jibu la kimfumo ili kuweza kung'oa kabisa mizizi ya ubaguzi huo. 

Ripoti hiyo imesema kuwa, kufumbiwa macho ubaguzi wa kimbari kumeimarisha dhulma na ukatili na imesisitiza ulazima wa kuchukuliwa hatua za haraka za kukomesha uhalifu uliokita mizizi na kukanyagwa haki za kiuchumi, kijamii, kiutamaduni, kiraia na kisiasa. Bachelet pia ametoa maagizao ya kurekebisha hali hiyo na amezitaka nchi zote kuyatekeleza ikiwa ni pamoja na kutoa fidia za ubaguzi wa kimbari wa kihistoria na vilevile kuchangia bajeti ya harakati za kupinga ubaguzi wa rangi kama ile ya Black Lives Matter (BLM). Ripoti hiyo ya Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa imesema: Katika nchi nyingi za Ulaya na America, raia wenye asili ya Afrika wanaishi katika hali mbaya ya umaskini na wanakabiliana na vizuizi vingi katika nyanja za kupata elimu, huduma za afya, ajira, kushirikishwa katika masuala ya kisiasa na haki nyingine za kimsingi za binadamu.

Michelle Bachelet 

Ubaguzi wa kimbari na ukatili unaofanywa dhidi ya watu weusi katika historia ya nchi za Magharibi vina historia ndefu ya mamia ya miaka. Katika kipindi cha karne kadhaa za ukoloni wao barani Afrika, wazungu wa Ulaya waliwachukua mamilioni ya Waafrika kama watumwa na kuwatumikisha katika kazi za sulubu kwenye makoloni yao hususan huko kaskazini mwa America na Amaerica ya Latini. Hata hivyo ubaguzi wa rangi umekita mizizi zaidi katika nchi ya Marekani ambayo viongozi wake wanajinadi kuwa vinara wa kutetea haki za binadamu na uhuru. Kwa mfano tu ubaguzi na ukatili wa polisi ya Marekani dhidi ya raia weusi wanaounda asilimia 14 ya jamii ya watu wa nchi hiyo, sasa limekuwa tatizo kubwa na lililokita mizizi katika jamii ya Marekani. Licha ya kwamba harakati ya kupigania haki za kiraia za watu weusi katika muongo wa 1950 iliibua wimbi kubwa la kutetea haki za jamii hiyo na kupinga ubaguzi wa rangi, lakini yanayojiri nchini humo yanaonesha kwamba, ubaguzi bado ungalipo katika sekta na maeneo mbalimbali ya Marekani, na watu weusi wanaendelea kunyanyaswa na kubaguliwa na hata kuuliwa kwa sababu tu ya rangi ya ngozi yao.

Ukatili wa polisi ya Marekani dhidi ya raia weusi wa nchi hiyo hususan baada ya mauaji yaliyofanywa na polisi mzungu dhidi ya George Floyd tarehe 25 Mei mwaka jana huko katika mji wa Minnesota ambayo yalizusha malalamiko na maandamano katika pembe mbalimbali za dunia, umelifanya suala hilo limulikwe zaidi katika medani ya kimataifa. Baada ya mauaji ya George Floyd, Idara ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa iliamrishwa kutayarisha ripoti kamili kuhusu ubaguzi wa rangi wa kimfumo, ukiukaji wa haki za binadamu unaofanyika kwa mpangilio maalumu unaofanywa na taasisi za serikali dhidi ya watu weusi na misimamo ya serikali kuhusu maandamano ya amani ya kupinga ubaguzi. Ripoti ya sasa ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa pia imetolewa siku kadhaa tu baada ya mahakama ya Marekani kumpata na hatia ya mauaji polisi mzungu aliyehusika na mauaji ya Floyd, Derek Chauvin. Polisi huyo amehukumiwa kifungo cha miaka 22 na nusu jela kwa hatia ya mauaji hayo.

Polisi mzungu akimuua George Floyd

Samaneh Akwan, mchambuzi wa masuala ya Marekani anasema: "Ubaguzi wa rangi nchini Marekani unafanyika kimfumo; na wakati mtu kama Donald Trump anapata waungaji mkono kwa kutumia kaulimbiu za kibaguzi na hatimaye kushinda kiti cha raia wa Marekani, suala hilo huwa ni alama kwamba, fikra za ubaguzi na kujiona bora wazungu haziwezi kung'olewa kirahisi nchini Marekani; kwa sababu baadhi ya wazungu hao kamwe hawatawakubali watu weusi."

Nukta ya kuongezea hapa ni kuwa kimsingi fikra za Kimagharibi zinahubiri ubaguzi wa rangi na kuwaona watu weusi kuwa ni raia wa daraja la pili.    

Tags