Magaidi sita wa ISIS watiwa mbaroni magharibi mwa Iraq
Mkuu wa Idara ya Intelijensia na Kupambana na Ugaidi katika mkoa wa Anbar magharbii mwa Iraq ametangaza habari ya kutiwa mbaroni wanachama sita wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS).
Ahmad Faris amenukuliwa na shirika la habari la Tasnim akisema hayo na kuongeza kuwa, magaidi hao wa ISIS wamekamatwa usiku wa kuamkia leo katika operesheni iliyofanyika katika mkoa wa Anbar.
Katika miezi ya karibuni, mashambulizi ya kundi la kigaidi la Daesh yameongezeka hususan katika maeneo kati ya mikoa ya Kirkuk, Salahuddin na Diyala.
Vyombo vya usalama nchini humo vimeshadidisha operesheni za kiusalama kwa ajili ya kuyasambaratisha mabaki ya Daesh katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Hivi karibuni, harakati ya muqawama wa Kiislamu ya An-Nujabaa ya Iraq ilitoa mkanda wa video unaoonyesha jinsi helikopta za jeshi la Marekani zinavyowahamisha kutoka Syria na kuwapeleka Iraq magaidi wa kundi la ukufurishaji la Daesh (ISIS).