Palestina: Ujenzi wa vitongoji vya Wazayuni unaendelea Ukingo wa Magharibi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i63783-palestina_ujenzi_wa_vitongoji_vya_wazayuni_unaendelea_ukingo_wa_magharibi
Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imetangaza kuwa, utawala wa Kizayuni unaendeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, tofauti kabisa na madai ya Imarati na Bahrain ya kusimamishwa ujenzi wa vitongoji hivyo baada ya nchi hizo mbili za Kiarabu kutangaza uhusiano wa kawaida na Israel.
(last modified 2026-01-14T11:42:18+00:00 )
Oct 03, 2020 02:42 UTC
  • Palestina: Ujenzi wa vitongoji vya Wazayuni unaendelea Ukingo wa Magharibi

Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imetangaza kuwa, utawala wa Kizayuni unaendeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, tofauti kabisa na madai ya Imarati na Bahrain ya kusimamishwa ujenzi wa vitongoji hivyo baada ya nchi hizo mbili za Kiarabu kutangaza uhusiano wa kawaida na Israel.

Mtandao wa habari wa "Arab 48" umeinukuu Wizara ya Mambo ya Nje wa Palestina ikisema katika taarifa yake ya jana Ijumaa kwamba, utawala wa Kizayuni umezidisha ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi kama sehemu ya utekelezaji wa mpango khabithi wa "Muamala wa Karne" na mpango mwengine wa kupora maenezo zaidi ya Wapalestina ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Wizara ya Mambo ya Nje wa Palestina imesisitiza pia kuwa, utawala wa Kizayuni umezidisha ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni huku Marekani na Israel zikiendesha propaganda za uongo ili walimwengu wasijue ukweli wa mambo. Imesema, baadhi ya nchi za Kiarabu zimetumbukia kwenye shimo la mapatano na Wazayuni maghasibu kwa propaganda hizo.

Wasaliti wa kadhia ya Palestina wakitiliana saini uhusiano rasmi na Wazayuni makatili

 

Hivi karibuni utawala wa Kizayuni ulitangaza kuwa, umekusudia kupora asilimia 30 nyingine ya ardhi za Wapalestina za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Hata hivyo kutokana na upinzani mkali uliooneshwa na wananchi na makundi ya Palestina, hadi hivi sasa utawala huo vamizi umeshindwa kutekeleza kivitendo nia yake hiyo khabithi.

Hata hivyo, Israel imezidisha ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kwenye ardhi nyingine ulizowapora Wapalestina katika hali ambayo, tarehe 25 Septemba, mawaziri wa mambo ya nje wa Imarati na Bahrain walitangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni kwa madai eti Israel itaacha kupora ardhi za Wapalestina.