Yemen yasisitiza kukabiliana na ugaidi wa kimataifa unaoongozwa na Marekani
Mjumbe wa Baraza la Kisiasa la Yemen amesisitiza kuwa, nchi hiyo itakabiliana na ugaidi wa kimataifa unaoongozwa na Marekani.
Muhammad Ali al-Houthi ameandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba "wakati nchi 17 zinaendelea kuiwekea mzingiro Yemen na wakati ripoti ya Benki ya Dunia inaeleza kwamba watoto milioni mbili Wayemen wanateseka kwa lisheduni, sisi, tukiwa watu tunaotetea uhuru, tunapaswa kufanya juhudi na kutumia kila wenzo kukabiliana na ugaidi wa kimataifa unaoongozwa na Marekani na washirika wake."
Al-Houthi amebainisha kuwa, kila mtetezi wa uhuru anapaswa kushiriki katika kampeni inayoendeshwa kwa anuani ya #"Mzingiro Dhidi ya Yemen ni Jinai ya Kigaidi".
Mnamo mwezi Machi 2015, Saudi Arabia, ikiungwa mkono na Marekani, Imarati na nchi nyingine kadhaa iliivamia kijeshi Yemen na kuiwekea nchi hiyo mzingiro wa nchi kavu, baharini na angani.
Moto wa vita uliowashwa na Saudia na washirika wake, hadi sasa umeshateketeza roho za Wayemeni zaidi ya 16,000 na kuwajeruhi makumi ya maelfu ya wengine, mbali na mamilioni waliolazimika kuwa wakimbizi.
Uvamizi wa kijeshi uliofanywa na muungano unaoongozwa na Saudia umeisababishia pia nchi masikini ya Yemen uhaba mkubwa wa chakula na dawa.../