UN: Uchunguzi ufanyike baada ya moto kuua watu 82 hospitalini Baghdad
Umoja wa Mataifa umetaka uchunguzi ufanyike kuhusu moto uliozuka hospitalini na kupelekea watu 82 kupoteza maisha katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad.
Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq, Jeanine Hennis-Plasschaert, ametuma salamu za rambirambi kwa familia za waliopoteza maisha katika mkasa huo wa moto huku akiwatakia ahueni ya haraka majeruhi.
Umoja wa Mataifa umeelezea mshtuko wake na machungu makubwa kufuatia vifo vya watu 82 waliopoteza maisha baada ya moto mkubwa kulipuka katika hospitai ya Ibn al-Khatib inayotibu wagonjwa wa COVID-19 kwenye mji mkuu wa Iraq, Baghdad. Mwakilishi huyo wa Umoja wa Mataifa ametaka hatua madhubuti zikuchukuliwe ili kuzuia tukio kama hilo kujikariri katika siku za usoni.
Hospitali hiyo iliwaka moto usiku wa Jumamosi ambapo zaidi ya watu 100 wameripotiwa kujeruhiwa, huku vyombo vya habari vikidai kuwa chanzo cha moto ni mlipuko wa mtungi wa hewa ya oksijeni.
Waziri Mkuu wa Iraq, Mustafa al-Kadhimi amemsimamisha kazi waziri wa afya na kuagiza uchunguzi wa tukio hilo ufanyike haraka huku akitangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa. Watu zaidi ya 100 wamejeruhiwa katika tukio hilo ambalo limeibua hasira na kupelekea kusimamishwa kazi baadhi ya maaafisa wakuu wa sekta ya afya nchini humo.