Imran Khan aitaka OIC kupambana na propaganda chafu dhidi ya Uislamu
-
Imran Khan
Waziri Mkuu wa Pakistan amezitaka nchi wanachama katika Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kupambana ipasavyo na wimbi la propaganda chafu dhidi ya Uislamu (Islamophobia) na kusema, ni makosa na ukosefu wa uadilifu kuufungamanisha Uislamu na ugaidi.
Imran Khan ameyasema hayo katika mazungumzo yake na mabalozi wa nchi wanachama wa OIC mjini Islamabad na kuzitolea wito nchi hizo kufanya mapambano endelevu na ipasavyo dhidi ya propaganda zinazopiga vita Uislamu na kuchafua sura safi ya dini hiyo.
Waziri Mkuu wa Pakistan amesema kuwa, matusi na maneno yanayomvunjia heshima Mtume Muhammad (saw) yanawaathiri na kuwaumiza sana Waislamu bilioni 1.5, na nchi za Waislamu haiwezi kuukinaisha Ulimwengu wa Magharibi kwamba jambo hilo, yaani matusi, halina uhusiano wowote na uhuru wa kusema na kujieleza.
Imran Khan pia ameitaka Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kufanya jitihada kubwa za kuijulisha jamii ya kimataifa kuhusu mapenzi na heshima kubwa ya Waislamu kwa Mtume Muhammad (saw) na Qur'ani tukufu.
Matamshi ya Waziri Mkuu wa Pakistan katika kikao cha mabalozi wa nchi za Kiislamu kilichofanyika Islamabad kuhusu ulazima wa kukabiliana na propaganda chafu dhidi ya Uislamu yanabainisha uhakika kwamba, kuzembea kwa nchi za Kiislamu katika suala la kukabiliana na hujuma na propaganda chafu zinazofanywa katika nchi za Magharibi dhidi ya Uislamu na matukufu yake kutazidisha au kushajiisha ushetani wa maadui wa dini hiyo.
Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi kwa kipindi cha zaidi ya muongo mmoja sasa zimekuwa zikieneza propaganda chafu dhidi ya Uislamu katika fremu ya kutekeleza ajenda yao ya kuzishinikiza nchi za Waislamu; suala ambalo limezusha wimbi kubwa la hujuma na mashambulizi dhidi ya Waislamu na maeneo yao ya ibada katika pembe mbalimbali za dunia.
Matamshi ya Imran Khan kuhusu udharura wa kupambana na hujuma na propaganda chafu dhidi ya Uislamu yamejikita zaidi katika nukta mbili. Mosi ni kwamba, kuuhusisha ugaidi na Waislamu kuna lengo la kchafua sura safi ya dini ya Uislamu na kuitangaza kuwa ni dini ya kikatili na utumiaji wa mabavu ili kupitia njia hiyo, Marekani na waitifaki wake waweze kuhalalisha mashambulizi na uvamizi wao katika baadhi ya maeneo ya dunia hususan nchi za Kiislamu.
Pili ni kwamba, kupitia ajenda hiyo ya kuwapachika Waislamu sifa ya ugaidi na ukatili, nchi hizo zinatayarisha mazingira ya kuwanyima Waislamu haki zao za mtu binafsi na za kijamii katika nchi za Magharibi, kuwafukuza na hata kuwatenga katika jamii zisizo za Kiislamu.
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Kiislamu ya Haki za Binadamu nchini Uingereza (IHRC) Massoud Shajareh anasema: Hujuma na propaganda chafu dhidi ya Uislamu (Islamophobia) ni sehemu ya ukweli mchungu unaoshuhudiwa katika nchi za Magharibi. Vyombo vya habari na wanasiasa ndio wanaochochea moto wa propaganda za kuchafua sura na jina la Uislamu na wamekuwa wakitunga sheria dhidi ya ugaidi wakiulenga Uislamu na Waislamu na hivyo kuhalalisha hujuma dhidi ya dini hiyo na utamaduni wa Waislamu.
Sera hizo za kuchafua sura na jina la Uislamu za Wamagharibi zimepelekea kuhalalishwa dhulma na manyanyaso dhidi ya wafuasi wa dini hiyo katika nchi za Magharibi na hata kukabiliwa na hujuma za makundi yenye misimamo mikali.
Sehemu ya siasa hizo za kuhujumu Uislamu katika miaka ya karibuni zimefanyika katika sura ya kuvunjia heshima matukufu ya Waislamu ikiwa ni pamoja na uchoraji wa vibonzo vinavyomvunjia heshima Mtume Muhammad (saw) nchini Ufaransa mwaka jana wa 2020. Vitendo kama hivyo ni kielelezo cha kuvunjia heshima matukufu ya dini na kudharau na kukejeli itikadi zao za kidini.
La kusikitisha ni kuwa, baada ya kuchapishwa vibonzo hivyo vinavyomvunjia heshima na kumtusi Mtume Muhammad (saw), Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alitoa matamshi ya kifidhuli akisema kuwa, uchapishaji wa vibonzo hivyo utaendelezwa nchini humo, suala ambalo limekabiliwa na upinzani mkali wa Waislamu kote duniani.
Katika hali hii ambapo Wamagharibi wanaendelea kutekeleza ajenda ya kuhujumu Uislamu, inatazamiwa kuwa, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) itachukua msimamo imara wa kukabiliana na hujuma hiyo ikiwa ni pamoja na kususia bidhaa zinazozalishwa katika nchi zinazofanya propaganda chafu na kuuhujumu Uislamu. Hatua nyingine inayoweza kuchukuliwa na nchi za Waislamu kukabiliana na hujumua hiyo ni pamoja na kutazama upya uhusiano wao wa kisiasa, kiuchumi na kibiashara na nchi zinazounga mkono na kuhamasisha vita na propaganda chafu dhidi ya Uislamu.