MSF: Gaza inasumbuliwa na uhaba wa dawa na huduma za tiba
Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) limetangaza kuwa, eneo la Ukanda wa Gaza linasumbuliwa na uhaba mkubwa wa dawa kutokana na mashambulizi ya jeshi la utawala wa Israel na mzingiro wa utawala huo dhidi ya eneo hilo.
Mkuu wa Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF), Helen Peterson amesema kuwa mzingiro na mashambulizi ya ndege za kivita za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza yamesababisha uhaba mkubwa wa dawa katika eneo hilo na kwamba, mgogoro huo wa dawa umezidisha changamoto ya kukabiliana na maambukizi ya corona.
Helen Peterson amesema kuwa, haijulikani hadi lini mfumo wa tiba na afya wa Gaza utaweza kustahamili mashambulizi ya mabomu ya utawala wa Israel.
Mkuu wa Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) amesema madaktari wawili wa shirika hilo tayari wameuawa katika mashambulizi ya Israel dhidi ya raia wa Ukanda wa Gaza.

Peterson ameitaka dunia itoe misaada ya haraka kwa ajili ya kufidia hasara na uharibifu mkubwa uliosababishwa na mashambulizi ya Israel katika vituo na taasisi za huduma za afya za shirika hilo katika Ukanda wa Gaza.
Kwa siku ya nane sasa jeshi la utawala haramu wa Kizayuni wa Israel linafanya mashambulio ya kinyama dhidi ya eneo la Ukanda wa Gaza, ambapo ripoti za karibuni kabisa zinaeleza kwamba Wapalestina wanaokaribia 200 wameshauwa shahidi hadi sasa wakiwemo watoto 58 na wanawake 34.