Jun 11, 2021 12:30 UTC
  • Wananchi Bahrain waandamana kulaani kifo cha mfungwa wa kisiasa gerezani

Mamia ya Wabahraini wamejitokeza kuandamana katika mji mkuu Manama, kumkumbuka mfungwa wa kisiasa ambaye amefariki dunia kutokana na COVID-19 akiwa katika gereza la kuogofya la utawala wa kiimla wa Aal Khalifa.

Maandamano hayo yalifanyika Jumatano na Alhamisi usiku ambapo waandamanaji wamelalamikia kifo cha Hussein Barakat, ambaye alikuwa mfungwa wa kisiasa aliyepoteza maisha baada ya kuambukizwa COVID-19 akiwa gerezani. Kijana Barakat alikuwa mwanaharakati wa Kiislamu ambaye alikuwa anashikiliwa katika gereza la kuogofya la Jau kusini mwa Manama ambapo wakuu wa gereza hilo walikataa kumpa matibabu.

Waandamanaji hao wamelaani utawala wa Aal Khalifa kwa kumuua shahidi mfungwa huyo wa kisiasa ambaye alikuwa Muislamu wa madhehebu ya Shia.

Tangu Februari mwaka 2011, wakati ulipoanza mwamko wa Kiislamu Asia Magharibi, Bahrain imekuwa uwanja wa maandamano ya amani ya wananchi wanaopinga utawala wa kifalme wa ukoo wa Aal Khalifa.

Maandamano dhidi mfalme wa Bahrain Hamad bin Isa bin Salman Al Khalifa

Wananchi hao wanataka kuwepo uhuru, uadilifu, kukomeshwa ubaguzi na kuundwa serikali itakayochaguliwa na wananchi wenyewe.

Hata hivyo kwa msaada wa wanajeshi wa Saudi Arabia na askari usalama wa Imarati waliotumwa nchini Bahrain kupitia mpango wa ulinzi wa Ngao ya Kisiwa, utawala wa Aal Khalifa unatumia mkono wa chuma kukabiliana na matakwa ya wananchi hao.

Kwa mujibu wa duru za haki za binadamu, Bahrain ina idadi kubwa zaidi ya wafungwa wa kisiasa kulinganisha na idadi ya watu katika nchi hiyo ndogo zaidi katika Ghuba ya Uajemi.

Tags