UN yailaumu serikali ya Imarati kwa kuvunja haki za binadamu
Mary Lawlor, mwakilishi wa ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa ameelezea kusikitishwa sana na utiaji watu mbaroni na uvunjaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanyika katika Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na kutaka kuachiliwa huru haraka watu wanaowekwa kizuizini kiholela.
Shirika la habari la IRNA limeripoti habari hiyo na kusema kuwa, wanaharakati kadhaa wa haki za binadamu walikamatwa nchini Imarati mwezi Julai 2013 kwa tuhuma za kufanya njama za kuipindua serikali ya Abu Dhabi na hivi sasa wametwishwa kifungo cha miaka 10 jela.
Taarifa ya ofisi ya Mary Lawlor, mwakilishi wa ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa aliyeko chini ya Kamisheni Kuu ya umoja huo katika masuala ya haki za binadamu imesema kuwa, adhabu iliyotolewa kwa wanaharakati hao ni kubwa sana tena kwa watu ambao walikuwa wanafanya kazi zao rasmi, kwa uwazi na kwa mujibu wa sheria.
Vile vile amesema, kuna ripoti za kutia hofu zinazohusu kufungwa watu hao kwa muda mrefu katika seli za mtu mmoja mmoja. Ripoti nyingine zinasema kuwa wanaharakati hao wanazimiwa mashine za kusafisha na kufanya baridi hewa tena wakiwa kwenye joto la zaidi ya daraja 40. Wanawekwa kwenye seli zilizofungwa madirisha, wananyimwa haki yao ya kufaidika na mwanga wa jua na ripoti nyingine mbalimbali ambazo zinatia hofu sana.
Malalamiko mengine yaliyotolewa na Umoja wa Mataifa ni kuhukumiwa watu hao bila ya kupewa haki yao ya washauri wa sheria wa kuweza kuwatetea ipasavyo na huo ni uvunjaji mwingine mkubwa wa haki za kibinadamu za watu hao. Ndio maana Umoja wa Mataifa umeutaka Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) uwaachilie huru wanaharakati hao ili waweze kuendelea na majukumu yao ya kutetea haki za binadamu.