Mlingano wa Quds na makundi ya muqawama Magharibi mwa Asia
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i71414-mlingano_wa_quds_na_makundi_ya_muqawama_magharibi_mwa_asia
Harakati ya Kata'ib Hizbullah (Brigedi za Hizbullah) ya Iraq imetoa taarifa na kuashiria kuendelea jinai na chokochoko za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina na mji wa Quds (Jerusalem) na kutangaza rasmi kuingia katika kadhia ya 'Mlingano wa Quds' kwa lengo la kukabiliana na utawala wa Kizayuni wa Israel.
(last modified 2026-07-03T11:45:53+00:00 )
Jun 18, 2021 21:55 UTC
  • Mlingano wa Quds na makundi ya muqawama Magharibi mwa Asia

Harakati ya Kata'ib Hizbullah (Brigedi za Hizbullah) ya Iraq imetoa taarifa na kuashiria kuendelea jinai na chokochoko za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina na mji wa Quds (Jerusalem) na kutangaza rasmi kuingia katika kadhia ya 'Mlingano wa Quds' kwa lengo la kukabiliana na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kwa miongo kadhaa sasa, mji wa Quds umekuwa ni kitovu cha makabiliano na vita baina ya utawala haramu wa Israel na makundi ya kupigania ukombozi wa Palestina au muqawama. Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, Quds imekuwa na umuhimu katika mapambano baina ya Israel na makundi ya muqawama kutokana na misimamo ya Donald Trump rais aliyeondoka wa Marekani.

Mnamo Disemba 2017, Trump alichukua maamuzi yaliyo kinyume cha sheria ambapo aliutangaza mji wa Quds kuwa ni mji mkuu wa utawala bandia wa Israel. Kwa msingi huo,  mnamo Mei 2018, Trump alitangaza kuuhamisha ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv hadi Quds, hatua ambayo ililaaniwa vikali kimataifa ambapo hata waitifaki wa Marekani nao pia walipinga uamuzi huo.

Hatua hiyo ya Trump imepelekea Israel iwe na ndoto na dhana potovu kuwa ndiye mmiliki wa Quds Tukufu na hivyo imekithirisha jinai zake dhidi ya Wapalestina wanaoishi katika mji huo.

Jinai za utawala wa Israel katika eneo la Sheikh Jarrah mjini Quds, ambako utawala huo umekuwa ukitekeleza njama ya kupora nyumba na ardhi za Wapalestina, ndio kilichokuwa chanzo cha vita vya hivi karibuni vya siku 12 vya utawala huo katili dhidi ya Ghaza. Hata baada ya vita hivyo vya mwezi Mei kumalizika, lakini bado utawala wa Kizayuni wa Israel unaendeleza ukatili na jinai dhidi ya Wapalestina wanaoishi mjini Quds.

Wapiganaji wa  Kata'ib Hizbullah (Brigedi za Hizbullah) ya Iraq 

Utawala pandikizi wa Israel unatekeleza jinai hizo katika hali ambayo, hata makundi ya mhimili wa muqawama au mapambano ya Kiislamu yameouonya utawala huo kuwa kuendelezwa jinai dhidi ya Quds na wakaazi wake ni jambo ambalo litaibua vita vya kieneo.

Kwa maeneno mengine ni kuwa, jinai za Israel dhidi ya Wapalestina mjini Quds na halikadhalika hujuma dhidi ya Msikiti wa Al Aqsa hazitaishia tu katika makabiliano ya askari wa Israel na harakati za ukombozi wa Palestina, bali wigo wa mapigano sasa utachukua muelekeo wa kieneo ambapo makundi ya muqawama yatakabiliana ana kwa ana na Israel.

Ni kwa msingio huo ndio Sayyid Hassan Nasrallah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon alipozungumza baada ya kumalizika vita vya Israel dhidi ya Ghaza ambavyo vilipewa lakabu ya 'Upanga wa Quds' alitangaza kuibuka mlingano mpya katika eneo. Sayyid Nasrallah aliuhutubu utawala wa Kizayuni wa Israel na kuuonya vikali utawala huo kuwa, kuendelea kuhujumu matukufu ya kidini katika mji wa Quds unaokaliwa kwa mabavu kutapelekea kuibuka vita kieneo.

Sayyid Hassan Nasrallah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon

Inaonekana wazi kwamba indhari ya Sayyid Hassan Nasrallah sasa imeondoka katika maeneo na inaelekea kutekelezwa kivitendo. Ni kwa msingi huo ndio maana Harakati ya Kata'ib Hizbullah (Brigedi za Hizbullah) ya Iraq ikawa kundi la kwanza la muqawama kutangaza rasmi kuingia katika mlingano wa Quds kwa ajili ya kushirikiana na makundi ya muqawama ya Palestina katika vita na utawala wa Kizayuni wa Israel. Katika taarifa yake, Harakati ya Kata'ib Hizbullah imesisitiza kuwa itafungamana na ahadi yake ya kulinda matukifu ya Kiislamu kufuatia kauli ya Sayyid Hassan Nasrallah kuwa 'kila hatari inayoikabili Quds itakuwa na maana ya vita vya kieneo."

Uamuzi huo wa Harakati ya Kata'ib Hizbullah ya Iraq ya bila shaka utachukuliwa pia na harakati zingine za muqawama katika eneo na kwa hakika maamuzi kama hayo ni kati ya matokeo ya  vita vya 'Upanga wa Quds'.

Weledi wa mambo wanaamini kuwa, mapigano ya 'Upanga wa Quds' yameleta mlingano mpya katika eneo hili katika makabiliano na utawala wa Kizayuni wa Israel. Kuingia Harakati ya Kata'ib Hizbullah ya Iraq katika  mlingano wa Quds ni jambo linaloashiria mshikamano baina ya makundi ya muqawama katika eneo na hivyo kuendelea jinai za Israel dhidi ya Wapalestina kutakuwa na gharama kubwa kwa utawala huo kama ambavyo vita vya siku 12 viliudhoofisha zaidi utawala huo ghasibu.