Wasiwasi waongezeka, Wazayuni wakijiandaa kufanya maandamano 14 ya kichochezi leo Jumatatu
Baada ya walowezi wa Kizayuni kutangaza nia yao ya kufanya maandamano 14 ya kichochezi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan leo Jumatatu, kamati za muqawama za wananchi wa Palestina nazo zimetoa mwito kwa Wapalestina kujitokeza katika medani ya kupambana na chokochoko za Wazayuni hao.
Kwa mujibu wa shirika la habari la FARS, kamati za muqawama wa wananchi wa Palestina zimetoa mwito kwa Wapalestina wanaoishi kwenye Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu tangu mwaka 1948 zilizopachikwa jina bandia la Israel, kujitokeza kwa wingi leo Jumatatu kukabiliana na maandamano 14 ya kichochezi ya Wazayuni yaliyopewa jina la "Maandamano ya Bendera."
Jumanne iliyopita pia walowezi wa Kizayuni walifanya maandamano mengine kama hayo ili kuwachochea Wapalestina. Lengo la maandamano hayo ya Wazayuni ni kuwashinikiza viongozi magaidi wa Israel kuongeza kasi ya kubomoa nyumba za Wapalestina na kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni.
Jana Jumapili pia, walowezi wa Kizayuni walikivamia Kibla cha Kwanza cha Waislamu yaani Msikiti wa Al Aqsa katika mji wa Baytul Muqaddas au Quds huku wakilindwa na askari wa utawala haramu wa Israel.
Shirika la Habari la Felestin al Youm, liliripoti kuwa, Wazayuni hao wenye misimamo mikali waliingia kwenye maeneo mbali mbali ya wazi ya Msikiti wa al Aqsa huku wakitoa maneno ya kejeli dhidi ya Uislamu na Waislamu.
Utawala pandikizi wa Israel unafanya jinai hizo katika hali ambayo, makundi ya muqawama au mapambano ya Kiislamu yameuonya utawala huo kuwa, kuendelezwa jinai dhidi ya Quds na wakaazi wake ni jambo ambalo litazusha vita vikubwa katika ukanda huu wote kwani Waislamu hawawezi kuvumilia jinai za Wazayuni hao.