Emir wa Qatar azungumza kwa simu na rais mteule wa Iran
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i71642-emir_wa_qatar_azungumza_kwa_simu_na_rais_mteule_wa_iran
Emir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani amefanya mazungumzo ya simu na rais mteule wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Seyyed Ebrahim Raeisi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 25, 2021 03:14 UTC
  • Emir wa Qatar azungumza kwa simu na rais mteule wa Iran

Emir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani amefanya mazungumzo ya simu na rais mteule wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Seyyed Ebrahim Raeisi.

Katika mazungumzo hayo ya Alhamisi usiku, Emir wa Qatar amepongeza Raeisi kwa ushindi wake katika uchaguzi wa rais hivi karibuni nchini Iran huku akimtakia mafanikio katika kipindi cha uongozi wake.

Al Thani pia ameipongeza Iran kwa kuiunga mkono Qatar wakati ilipokuwa imewekewa mzingiro na Saudia na hasa amemshukuru Raeisi kwa nafasi yake katika kadhia hiyo wakati akiwa mkuu wa Idara ya Mahakama ya Iran. 

Kwa upande wake, Rais-mteule Raeisi amesisitiza haja ya kumalizika uingiliaji wa madola ya kigeni katika masuala ya eneo. Amesema usalama wa pamoja kieneo unaweza kupatikana iwapo madola ya kigeni yataondoka Asia Magharibi. 

Mapema wiki hii pia  Emir wa Qatar alimtumia Raeisi salamu za pongezi kufuatia ushindi wake katika uchaguzi wa rais na huku akimtakia mafanikio pia alielezea matumaini yake kuwa uhusiano wa Iran na Qatar utazidi kuimarika. 

Viongozi mbali mbali duniani wanaendelea kumtumia salamu za pongezi Sayyid Ebrahim Raeisi kufuatia ushindi wake katika uchaguzi wa rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uliofanyika Ijumaa iliyopita.

Raeisi alipata karibu asilimia 62 ya kura zote zilizopigwa katika uchaguzi huo  na ataapishwa mwezi Agosti kuchukua nafasi ya Rais Hassan Rouhani  ambaye anamaliza muhula wake wa pili baada ya kushikilia nafasi hiyo kwa muda wa miaka minane.

Rais mteule wa Iran Sayyed Ebrahim Raeisi

Viongozi wengine waliompongeza Rais mteule Raeisi ni pamoja na Rais Vladimir Putin wa Russia, Rais Muhamamdu Buhari wa Nigeria, Rais Bashar al Assad wa Syria, Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina. Rais Barham Salih wa Iraq,  Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki , Waziri Mkuu Imran Khan wa Pakistan, Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu Khalifa bin Zayed Aal Nahyan, Sultan wa Oman Haitham bin Tariq Aal Said , Rais wa Jamhuri ya Azerbaijan Ilham Aliyev, Rais Xi Jinping wa China, Rais Miguel Diaz Canel wa Cuba, Rais Abdul Majid Taboune wa Algeria, Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un, Rais Nicholas Maduro wa Venezuela. Rais Alezander Lukashenko wa Belarus na Rais wa Armenia Armen Sargsyan.