Hizbullah yalaani hatua ya Marekani kufunga tovuti za mrengo wa muqawama
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i71644-hizbullah_yalaani_hatua_ya_marekani_kufunga_tovuti_za_mrengo_wa_muqawama
Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imelaani vikali hatua ya serikali ya Marekani kuteka na kufunga tovuti kadhaa za vyombo vya habari vya Iran na kieneo na kusema kitendo hicho ni jinai inayothibitisha sera za ukandamizaji zinazofuatwa na Washington.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 25, 2021 03:19 UTC
  • Hizbullah yalaani hatua ya Marekani kufunga tovuti za mrengo wa muqawama

Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imelaani vikali hatua ya serikali ya Marekani kuteka na kufunga tovuti kadhaa za vyombo vya habari vya Iran na kieneo na kusema kitendo hicho ni jinai inayothibitisha sera za ukandamizaji zinazofuatwa na Washington.

Mkuu wa Ofisi ya Mahusiano ya Umma ya Hizbullah Mohammad Afif amesema kitendo hicho kiovu cha Marekani kinalenga kuficha ukweli kuhusu jinai ambazo imezitenda pamoja na waitifaki wake dhidi  ya watu wanaodhulumiwa katika eneo hasa watu wa Yemen na Palestina ambao wanakabiliwa na mzingiro mbaya zaidi.

Naye Qais Khazali, kiongozi wa Harakati ya Asa'ib Ahl al-Haq ya Iraq amelaani hatua ya Marekani kufunga tovuti za habari za Iran na harakati za muqawama katika eneo. Amesema kitendo hicho kinaweka wazi ukweli kuwa nchi za Magharibi zinahadaa zinapodai kutetea haki za binadamu na uhuru wa maoni. Amesema Marekani imeteka tovuti za habari ambazo zimekuwa zikipinga njama za Marekani, Uingereza, utawala wa Israel, Saudia na Imarati. Amesema kitendo hicho cha Marekani ni ithbati tosha kuwa imeshindwa kijeshi na sasa imeamua kupambana na fikra.

Juzi serikali mpya ya Marekani iliendeleza sera za kijuba na kibeberu za nchi hiyo kwa kuzifunga tovuti za televisheni za kimataifa za Iran na vyombo vya habari vya mrengo wa muqawama au mapambano ya Kiislamu Yemen, Palestina, Iraq na Bahrain.

Televisheni ya Kiingereza ya Iran ya Press TV na zile za Kiarabu za Al Alam na Al Khauthar ni kati ya vyombo vya habari ambavyo vimefungiwa tovuti zao na Marekani.

Kufuatia hatua hiyo Press TV imetangaza kuwa tovuti iliyofungwa ya presstv.com  sasa inapatikana kupitia presstv.ir