May 17, 2016 07:52 UTC
  • Kongamano la kupinga utawala wa Aal Saudi lafanyika nchini Syria

Shakhsia kadhaa wa kidini na kisiasa kutoka nchi kadhaa za eneo la Mashariki ya Kati wameshiriki kongamano la kuchunguza jinai za utawala wa Aal Saudi lililofanyika katika mji mkuu wa Syria Damascus.

Washiriki wa kongamano hilo lililofanyika kwa anuani ya "Utawala wa Saudia ni Gaidi" wamelaani jinai za kinyama zinazofanywa na utawala wa Aal Saudi dhidi ya wananchi wa mataifa ya Kiarabu na ya Kiislamu.

Kongamano hilo limeandaliwa na Muungano wa "Vijana wa Mapinduzi ya Februari 14" wa Bahrain kwa ushirikiano na harakati ya wananchi wa Iraq ya Al-Hashadu al-Sha'abi kwa lengo la kufichua na kuweka hadharani jinai za kinyama za utawala wa Aal Saudi nchini Syria na katika nchi nyengine za Kiarabu na za Kiislamu za eneo.

Shakhsia kutoka Iraq, Yemen, Bahrain pamoja na jumuiya za kidini na za wananchi za Syria zimeshiriki katika kongamano hilo.

Baadhi ya wazungumzaji katika kongamano la "Utawala wa Saudia ni Gaidi" wameashiria jinai za Aal Saudi dhidi ya wananchi wa mataifa ya eneo na kusisitiza kuwa fikra ya Uwahabi inapeleka maelfu ya magaidi nchini Iraq ili kufanya mauaji bila ya kutafautisha wafuasi wa madhehebu yoyote ile. Aidha wamebainisha kuwa fikra hiyo ya Uwahabi inaunga mkono ugaidi katika nchi ya Yemen na kuuunga mkono pia utawala dhalimu wa Bahrain unaowakandamiza wananchi wa nchi hiyo.

Katika kongamano hilo la Damascus, yamefanyika pia maonesho ya picha zinazoakisi jinai za utawala wa Saudia pamoja na harakati za utawala huo katika nchi za Syria, Iraq, Yemen na Bahrain.

Saudi Arabia, ikishirikiana na Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ndio waungaji mkono wakuu wa makundi ya kigaidi kama Daesh na al-Qaeda katika eneo.../

Tags