Iran na Syria mfano mzuri wa ushirikiano wa kistratijia kieneo
Iran na Syria zimechukua na zitaendelea kuchukua hatua muhimu katika kupambana na ugaidi wa kiuchumi kwa ajili ya kulinda maslahi ya watu wa nchi mbili hizi.
Hilo limesisitizwa na Hussein Amir Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambaye aliwasili nchini Syria Jumamosi baada ya kuzitembelea nchi za Russia na Lebanon.
Moja ya mambo yanayopewa kipaumbele katika sera za diplomasia ya serikali ya kumi na tatu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuboresha uhusiano na nchi za eneo kwa madhumuni ya kuimarisha usalama, uhusiano wa kiuchumi wa pande mbili na pande kadhaa na pia kuzihamasisha nchi za eneo zichukue hatua za kutatua kwa amani tofauti zao bila uingiliaji wa nchi za kigeni.
Stratijia hiyo imebadilisha masuala ya kiusalama na kijeshi kwa maslahi ya nchi za eneo. Kushindwa njama za Marekani na utawala haramu wa Israel pamoja na vibaraka wao wa kieneo, katika nchi za Syria na Iraq, njama ambazo kwa hakika zililenga kuzigawa nchi za eneo na kuweka mipaka bandia ya kijografia na kiutawala, ni moja ya matunda chanya yaliyopatikana katika uwanja huo.
Akizungumza na Hussein Amir Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Rais Bashar Asad wa Syria alisema kuondoka kwa madhila Marekani nchini Afghanistan ni alama ya kudhihiri mihimili mipya na kudidimia mhimili wa Magharibi. Amesema nchi za eneo na majirani wa Afghanistan wanafahamu fika kwamba Marekani haitakubali kubeba dhima ya uharibifu iliosababisha Afghanistan na kwa hivyo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapasa kushirikiana na nchi jirani na za eneo kwa ajili ya kurekebisha hali ya mambo katika nchi hiyo.
Hata kama Syria imepata mafanikio makubwa katika uwanja wa kupambana na magaidi wanaodhaminiwa kwa silaha na kifedha na nchi za Magharibi, lakini bado ina kazi kubwa ya kufanya kwa ajili ya kupambana na magaidi hao katika eneo la Idlib na kukomboa ardhi zake zingine zinazokaliwa kwa mabvu na nchi za kigeni. Ili kufikia lengo hilo inapasa kuongeza mapambano dhidi ya magaidi na kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa nchini. Ni wazi kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitaiacha pekee yake nchi hiyo katika suala hilo.
Abdel Bari Atwan, mchambuzi wa masuala ya kisiasa katika ulimwengu wa Kiarabu huku akisisitiza kuwa uwepo wa Iran nchini Syria ni wa kisheria, anasema kwamba uwepo huo unatuma ujumbe maalumu kwa Marekani na utawala ghasibu wa Israel pamoja na kudhihidrisha muungano wa kistratijia wa muda mrefu baina ya Iran na Syria na kwamba Marekani na Israel zisitarajie kuwa Iran itaondoka Syria karibuni.
Usahirikiano huo wa kistratijia kwa hakika ni jibu la kivitendo kwa sheria ya Marekani ya 'Caesar' ambayo inalenga kueneza baa la njaa Syria na kulemaza juhudi za ukarabati na ujenzi mpya nchini humo.
Taathira nyingine ya ushirikiano huo ni kuharakisha utekelezaji wa mikataba ya pande mbili kwa maslahi ya mataifa hayo. Iran, Syria, Iraq na Lebanon ambazo zimepitia kipindi kigumu na hatari cha vita na migogoro ya kieneo, sasa zinafanya juhudi za kuimarisha uhusiano na ushirikiano wao katika nyanja tofauti zikiwemo za biashara na uchumi.
Huku akisisitiza kuwa Iran na Syria zinaendeleza mazungumzo katika nyanya tofauti za kisiasa na kiuchumi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ametangaza habari ya kufanyika karibuni mjini Tehran safari ya Faisal Miqdad, waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Syria na kuongeza kuwa hiyo ni ishara tosha kwamba wizara mbili hizo zimeazimia kufanikisha kivitendo siasa za marais wa nchi mbili.
Kwa kutilia maanani safari na mikataba mingi iliyotiwa saini na viongozi wa ngazi za juu wa nchi mbili, jambo ambalo bila shaka linaashiria wazi uhusiano mkubwa uliopo kati ya Iran na Syria, tunaweza kusema kuwa sasa kuna ruwaza iliyobainika wazi katika njia ya ushirikiano wa kistratijia wa nchi mbili ikiwa ni kwa maslahi ya mataifa mawili na manufaa ya nchi zote za eneo.