Waziri Mkuu wa Israel: Sitaruhusu kuundwa nchi huru ya Palestina
Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ametangaza kuwa, madhali angali madarakani katu hataruhusu nchi huru ya Palestina iundwe au hata kufanyika mazungumzo ya kisiasa.
Naftali Bennett amesema hayo katika mahojiano maalumu aliyofanyiwa na majarida kadhaa ya lugha ya Kiebrania na kusisitiza kwamba, serikali yake katu haitasalimu amri na kukubali maafikiano yoyote yale yenye lengo la kumaliza mzozo na mvutano wa kisiasa na Wapalestina kama makubaliano ya Oslo.
Waziri Mkuu wa Israel amesisitiza kuwa, serikali yake itaendelea na msimamo wake wa kupingwa kuundwa nchi huru ya Palestina.
Amesema kama ninavyomnukuu: Madhali ningali madarakani, hakutapatikana kitu kinachojulikana kama makubaliano ya Oslo, na kama hilo litatokea basi ni wakati ambao yeye na baraza lake la mawaziri hawatakuwa madarakani.
Waziri Mkuu wa Israel anashikilia msimamo huo katika hali ambayo, kilio kikubwa cha Wapalestina na wapigania huru na haki ulimwengu nii kuundwa dola huru la Palestina mji mkuu wake ukiwa Baytul-Muqaddas.
Wapalestina wanaamini kuwa, kuongezwa kasi ya ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni unaofanywa na Israel katika maeneo ya Wapalestina kunazima ndoto ya kuundwa dola huru la Palestina.
Makundi na wanaharakkati mbalimbali wa Kipalestina wameikuwa wakisisitiza kuwa, jamii ya kimataifa inapaswa kuchukua hatua za maana katika kusukuma mbele juhudi za kuundwa dola huru la Palestina mji mkuu wake ukiwa Baytul Muqaddas.
Wajuzi wa mambo wanaamini kuwa, amani haiwezi kupatikana katika eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) bila ya kuundwa nchi huru ya Palestina na kurejea makwao wakkimbizi wote wa Kipalestina.