Saudia yamkamata mwakilishi wa Waislamu Warohingya katika OIC
Utawala wa Saudia umemkamata mwakilishi rasmi wa Waislamu Warohingya katika Jumuya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) katika mji mtakatifu wa Makka.
Shirika la Wafungwa wa Kiitikadi linalotetea haki za binadamu Saudi Arabia, limeandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa, Dr Abdullah Maarouf, kutoka jamii ya Waislamu Warohingya wanaokandamizwa Myanmar, ambaye anawakilisha jamii hiyo katika OIC na ambaye pia ni mkuu wa Kituo cha Kimataifa cha Rohingya amekamatwa mjini Makka.
Tukio hilo limejiri siku kadhaa baada ya askari wa Saudia kumkamata mtetezi mwingine wa haki za Waislamu Warohingya, Omar al Arkani ambaye anaishi Makka.
Haijabainika ni kwa nini utawala wa Saudia umeamua kuwakamata watetezi hao wa haki za Waislamu Warohingya.
Itakumbukwa kuwa wimbi jipya la mauaji, mashambulizi na ubakaji wa jeshi la Myanmar katika mkoa wa Rakhine kuwalenga Waislamu wa Rohingya, lilianza tarehe 25 Agosti mwaka 2017 ambapo zaidi ya Waislamu elfu sita waliuawa na wengine elfu nane kujeruhiwa. Aidha zaidi ya Waislamu wengine milioni moja wa jamii hiyo walilazimika kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh huku wengine wakipata hifadhi katika nchi kama vile India, Thailand na Malaysia.
Aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad Al Hussein aliesema kuwa uhalifu unaofanywa na Mabudha kwa himaya ya serikali nchini Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya ni mauaji ya kimbari.