Sana'a: Inaaibisha mvamizi kupendekeza azimio la vikwazo dhidi ya Yemen
Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya uokovu wa kitaifa ya Yemen amesema, ni aibu na kichekesho kuona mmoja wa wavamizi ndiye aliyependekeza azimio la vikwazo vipya dhidi ya nchi hiyo.
Siku ya Jumatatu, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliafiki kuendelezwa marufuku ya kuuziwa silaha harakati ya Ansarullah ya Yemen sambamba na kupitisha rasimu ya azimio iliyopendekezwa na Imarati lililotaka kupanuliwa wigo wa marufuku ya silaha waliyowekewa baadhi ya viongozi wa Ansarullah kwa kujumuisha pia harakati hiyo nzima ya muqawama ya wananchi wa Yemen
Hisham Sharaf Abdullah, Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya uokovu wa kitaifa ya Yemen amesema, maazimio yaliyopitishwa karibuni na Baraza la Usalama kuhusu hali ya Yemen yanagongana waziwazi na Hati ya Umoja wa Mataifa inayotilia mkazo haki ya kimaumbile ya kujihami ziliyonayo mataifa.
Hisham ameongeza kuwa, hatua za kujihami za Sana'a na kulengwa taasisi za kijeshi na hasasi za muungano vamizi wa Saudia na Imarati ni jibu la kutarajiwa kwa jinai za kivita na mauaji ya kimbari ambayo yamekuwa yakifanywa na muungano huo tangu Machi 26, 2015.
Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya uokovu wa kitaifa ya Yemen ameendelea kueleza kwamba, kupitishwa azimio na Baraza la Usalama ni matokeo ya fursa iliyonayo Imarati ya uanachama usio wa kudumu katika baraza hilo, ambapo kwa msaada wa wanachama wa kudumu imeanza kutwisha misimamo yake; na kwa sababu hiyo, mwanadiplomasia huyo mkuu wa serikali ya Sana'a amelitaka Baraza la Usalama liunge mkono jitihada zinazofanywa kwa lengo la kuitatua kadhia ya Yemen kwa njia za kisiasa na za amani na kuhitimishwa mzingiro iliowekewa nchi hiyo.../