Kuwait yajiondoa kwenye kongamano Bahrain kufuatia kushiriki Israel
Wasomi wa vyuo vikuu kutoka Kuwait wameamua kususia kongamano ambalo limeandaliwa na Chuo Kikuu cha Bahrain baada ya kubainika kuwa ujumbe kutoka utawala haramu Israel umealikwa kushiriki kikao hicho.
Jumuiya ya Vijana wa Kuwait Watetezi wa Quds imetangaza kupitia ukurasa wake wa Twitter kuwa, waliaondaa kongamano hilo walikuwa wameficha ushiriki wa utawala haramu wa Israel lakini baadaye ikabinika kuwa kuna washiriki kutoka utawala huo unaokalia kwa mabavu ardhi za Palestina.
Musab al Mutawa, mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana wa Kuwait Watetezi wa Quds amesema kujiondoa wasomi wa Kuwait katika kongamano hilo ni kwa mujibu wa sera rasmi ya Kuwait ya kupinga uanzishwaji uhusiano wowote wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel. Amesema msimamo kama huo wa Kuwait unalenga kuushinikiza utawala wa Kizayuni wa Israel unaokalia kwa mabavu ardhi za Palestina ukiwemo mji wa Quds Tukufu (Jerusalem). Mutawa amesisitiza kuwa Kuwait inaunga mkono harakati za Wapalestina kukomboa ardhi zao zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Wakati huo huo, Harakati wa Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, imepongeza hatua ya ujumbe huo wa Kuwait kujiondoa katika kongamano hilo la Bahrain ambalo linawashirikisha Wazayuni. Msemaji wa Hamas Hazem Qasem amesema misimamo kama hiyo ya Kuwait inaenda sambamba na hisia za Waislamu duniani. Mwezi Mei mwaka jana Bunge la Kitaifa la Kuwait lilipitisha kwa pamoja sheria ya kupiga marufuku uanzishwaji uhusiano au mapatano na utawala wa Kizayuni wa Israel.