Hamas yapongeza oparesheni ya kujitolea mhanga kijana wa Kipalestina
Makundi ya Palestina katika Ukanda wa Ghaza yameitaja oparesheni ya kufa shahidi iliyotekelezwa katika Msikiti wa al Aqsa kuwa ni jibu kwa jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel.
Wanajeshi wa wawili wa Kizayuni walijeruhiwa jana asubuhi katika oparesheni ya muqawama iliyofanywa na kijana wa Kipalestina huko Babul Huttah katika Msikiti wa al Aqsa. Baada ya tukio hilo, wanajeshi wa Kizayuni walimpiga risasi na kumuua shahidi kijana huyo Mpalestina.
Shirika la habari la Shahab la Palestina limeripoti kuwa, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imepongeza oparesheni hiyo ya kujitolea kufa shahidi ya jana asubuhi huko Quds inayokaliwa kwa mabavu; ambayo imepelekea kujeruhiwa wanajeshi wawili wa Kizayuni na kufa shahidi mtekelezaji wa oparesheni hiyo.
Naye Tariq Izzuddin msemaji wa harakati ya Jihad Islami katika Ukingo wa Magharibi ameitaja oparesheni hiyo kuwa ni jibu la kawaida na halali kwa jinai za Wazayuni na kutoa wito wa kuzidishwa mapambano katika ardhi zote za Palestina kwa ajili ya kuilinda Quds, Msikiti mtakatifu wa al Aqsa na damu za mashahidi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Amesisitiza kuwa, damu za mashahidi ndio inayotoa msukumo wa kuwafurisha maghasibu wa Kizayuni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.
Huku wakitumia visingizio mbalimbali, wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel kila siku huwauwa shahidi, kuwajeruhi au kuwatia nguvuni wananchi wanaodhulumika wa Palestina; ambapo katika kujibu jinai hizo, Wapalestina pia hutekeleza oparesheni mbalimbali dhidi ya Wazayuni.