Wanawake wa Kuwait: Sheria ya ukatili majumbani haitoi kinga kwa wanawake
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i81100-wanawake_wa_kuwait_sheria_ya_ukatili_majumbani_haitoi_kinga_kwa_wanawake
Wanaharakati wa masuala ya wanawake nchini Kuwait wanasema kuwa, kutotekelezwa sheria ya ukatili majumbani dhidi ya wanawake na kutokuweko azma ya kweli ya kuitekeleza ni mambo ambayo yameongeza vitendo vya unyanyasaji, ubakaji na ukatili dhidi ya wanawake nchini humo.
(last modified 2026-07-02T04:13:23+00:00 )
Mar 07, 2022 00:49 UTC
  • Wanawake wa Kuwait: Sheria ya ukatili majumbani haitoi kinga kwa wanawake

Wanaharakati wa masuala ya wanawake nchini Kuwait wanasema kuwa, kutotekelezwa sheria ya ukatili majumbani dhidi ya wanawake na kutokuweko azma ya kweli ya kuitekeleza ni mambo ambayo yameongeza vitendo vya unyanyasaji, ubakaji na ukatili dhidi ya wanawake nchini humo.

Mtandao wa habari wa Arabiy al-Jadid unaripoti kwamba, licha ya kupasishwa sheria ya kupiga marufuku unyanyasaji wa kijinsia na ukatili dhidi ya wanawake majumbani nchini Kuwait Agosti 2020, lakini mwaka uliopita wa 2021, ulishuhudia kuongezeka vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake.

Taarifa hiyo inaeleza kwamba, takwimu za vitendo vya ubakaji na ukatili majumbani dhidi ya wanawake nchini Kuwait ziliongezeka mno katika mwaka uliopita na kwamba, waliohusika na vitendo hivyo ni ndugu na jamaa wa karibu wa familia.

Sehemu nyingine ya taarifa ya wanaharakati hao inavituhumu vyombo vya usalama na mfumo wa mahakama wa kutotoa ushirikiano katika uandikishaji kesi za wahanga wa matukio hayo ya unyanyasaji wa kijinsia, ubakaji na ukatili majumbani na badala yake kutosheka na kuchukua ahadi kwa kisingizio cha ada na mazoea ya kijamii.

Bunge la Kuwait

 

Inaelezwa kuwa, asilimia 50 ya wahanga wa vitendo hivyo walilazimika kufuta mashtaka yao kutokana na mashinikizo ya maafisa usalama.

Pamoja na hayo, wanaharakati wa haki za wanawake nchini Kuwait wanasema kuwa, hata takwimu zinazotolewa za wahanga wa ukatili majumbani ni chache ikilinganishwa na uhalisia wa mambo.

Kuna wanawake wengi nchini Kuwait ambao ni wahanga wa vitendo hivyo kijamii na kifamilia hawako tayari kwenda kushtaki kutokana na kuogopa kwenda polisi na mahakamani kutokana na ada na mazoea ya kijamii na kifamilia.