Afisa wa Palestina: Bin Salman anauhami Uzayuni na ubeberu
-
Muhammad bin Salman
Kiongozi mmoja wa Harakati ya Wananchi kwa Ajili ya Ukombozi wa Palestina amesema kuwa mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia, Muhammad bin Salman, ni muungaji mkono wa ubeberu na Uzayuni katika eneo la Magharibi mwa Asia.
Katika mahojiano yake na jarida la Marekani la Atlantic, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia, Muhammad bin Salman alisema kuwa Riyadh haiioni Israel kuwa ni adui, bali inaitazama kama mshirika wake. Msimamo huu wa Mwana Mfalme wa Saudia umevikasirisha sana vyama na makundi ya kupigania uhuru ya Wapalestina.
Makundi mbalimbali ya ukombozii wa Palestina yamelaani hatua ya baadhi ya nchi za Kiarabu ya kuhalalisha uhusiano wa Waarabu na utawala ghasibu wa Israel na kuutaja kuwa ni sawa na kudunga jambia katika moyo wa kadhia ya Palestina.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran Press, Iyad Awadallah, mmoja kati ya viongozi wa chama cha Popular Front for the Liberation of Palestine amelaani msimamo wa Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia, Muhammad bin Salman kuhusiana na utawala wa Kizayuni wa Israel na kusema Bin Salman amesaidia utekelezaji wa mipango ya kibeberu na kizayuni katika eneo la Magharibi mwa Asia.

Awadallah ameongeza kuwa, Saudi Arabia inataka kuuwezesha utawala wa Kizayuni unaoikalia Quds kwa mabavu kulidhibiti eneo hilo.
Itakumbukwa kuwa, nchi nne za Kiarabu ambazo ni Imarati (UAE), Bahrain, Morocco na Sudan mwaka 2020 zilitia saini makubaliano ya kuanzisha uhusiano rasmi na utawala wa Kizayuni wa Israel, suala ambao limekabiliwa na wimbi la upinzani katika nchi za Kiarabu na Kiislamu.