Wapalestina walaani safari ya rais wa Israel nchini Uturuki
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i81218-wapalestina_walaani_safari_ya_rais_wa_israel_nchini_uturuki
Harakati za mapambano ya Kiislamu ambazo zinapigania ukombozi wa Palestina zimelaani vikali safari ya rais wa utawala haramu wa Israel Isaac Herzog nchini Uturuki wakati huu ambao Israel imeshadidisha hujuma dhidi ya Wapalestina.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 10, 2022 04:31 UTC
  • Wapalestina walaani safari ya rais wa Israel nchini Uturuki

Harakati za mapambano ya Kiislamu ambazo zinapigania ukombozi wa Palestina zimelaani vikali safari ya rais wa utawala haramu wa Israel Isaac Herzog nchini Uturuki wakati huu ambao Israel imeshadidisha hujuma dhidi ya Wapalestina.

Katika taarifa Jumatano, Harakati ya Jihadi Islami imelaani serikali ya Uturuki kwa kumkaribisha Herzog nchini humo na kusema safari hiyo inajiri sambamba na kuongezeka mashambulizi ya Israel dhidi ya Wapalestina katika Mji wa Quds (Jerusalem) na njama za Israel za kuuyahudisha mji huo. Jihad Islami imeongeza kuwa kitendo cha Uturuki kumkaribisha rais wa Israel ni usaliti kwa Quds na Palestina. Safari hii inaashiria kumpendelea adui na ni dhidi ya jihadi ya watu wa Palestina, imesema harakati ya Jihad Islami.

Nayo Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas imebainisha masikitiko yake kutokana na safari ya rais wa Israel nchini Uturuki. Katika taarifa Hamas imetoa wito kwa nchi za Kiarabu na Waislamu kutoupa utawala wa Kizayuni fursa ya kujipenyeza katika eneo. Aidha Hamas imesema inapinga vikali mawasiliano yoyote na adui anayekiuka matukufu ya Kiislamu na anayetekeleza njama za kuuyahudisha mji wa Quds na Msikiti wa Al Aqsa sambamba na kuwawekea mzingiro Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza.

Waandamanaji Uturuki wakiwa wamebeba bango lililoandikwa "Hatutaki wauaji katika nchi yetu" huku wakiwa wamebeba bendera ya Palestina katika maandamano ya kupinga safari ya rais wa utawala haramu wa Israel nchini humo

Aidha Hamas imesema utawala haramu wa Israel unaendelea kuwashikilia mateka maelefu ya Wapaletina mbali na kuwaua watoto na kuharibu nyumba za Wapalestina. Herzog aliwasili Uturuki Jumatano kwa lengo la kuimarisha uhusiano uliokuwa unazorota baina ya Israel na Uturuki. Jana wananchi wa Uturuki walifanya maandamano makubwa ya kupinga na kulaani safari ya Herzog nchini humo. Katika maandamano hayo ya jana Jumatano, wananchi wa Uturuki waliokuwa wamekusanyika katika Medani ya Taksim walichoma moto bendera za utawala haramu wa Israel na kulaani safari hiyo ya siku mbili ya rais wa utawala dhalimu wa Israel.