Utawala wa Saudia wawanyonga watu 81 ndani ya saa 24
Utawala wa Aal-Saud nchini Saudi Arabia katika kipindi cha saa 24 umetekeleza hukumu ya kifo kwa kuwanyonga wafungwa 81 waliokuwa wanahusishwa na madai ya ugaidi.
Shirika rasmi la habari la serikali ya Riyadh lilitangaza hayo jana Jumamosi na kueleza kuwa, miongoni mwa wafungwa walionyongwa wapo raia saba wa Yemen na mmoja wa Syria.
Kwa mujibu wa shirika hilo, wafungwa hao wanadaiwa kufanya jinai mbalimbali, kama vile mauaji na kuwa wanachama wa makundi fulani ya kigaidi. Kunyongwa watu 81 ndani ya muda wa saa 24 kumepiku idadi ya watu wote walionyongwa wa watawala wa Aal-Saud ndani ya mwaka mzima wa 2021 nchini Saudia.
Watawala wa Riyadh wanadai kuwa, makumi ya watu waliowanyonga walihusika na jinai mbalimbali kama vile kuua watu wasio na hatia wakiwemo wanawake na watoto, na eti kwa kuwa wanachama wa magenge ya kigaidi kama al-Qaeda na ISIS.
Habari zaidi zinaarifu kuwa, baadhi ya watu walionyongwa hadi kufa na watawala wa Riyadh walikuwa wanachama wa harakati ya Ansarullah ya Yemen.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema kuwa, Saudi Arabia ni miongoni mwa nchi zinazoongoza dunia kwa kunyonga watu na imekuwa ikilaumiwa sana kutokana na rekodi yake mbaya ya kukanyaga haki za binadamu na kuwanyonga wafungwa wa kisiasa, wanaharakati na wapinzani kwa tuhuma zisizo na msingi kama ugaidi na kadhalika.