Jun 02, 2016 03:33 UTC
  • Mfalme wa Saudia akumbwa na matatizo ya kiakili, haruhusiwi kuona wageni

Mfalme Salman bin Abdulaziz wa Saudi Arabia amekumbwa na maradhi mabaya mno ya kiakili kiasi kwamba wageni wanazuiwa kumtembelea. Mwanae Mfalme Salman ambaye pia ni Waziri wa Ulinzi na Naibu Mrithi Kiti cha Ufalme, Mohammad bin Salman ametoa amri ya kupiga marufuku wageni kumtembelea baba yake ambaye ana maradhi sugu ya kiakili.

Kwa mujibu wa gazeti la mtandaoni la Kipalestina la Manar toleo la Jumatano, duru mjini Riyadh zinadokeza kuwa, wageni kutoka nchi za nje na hata watu wa ukoo wa kifalme wa Aal Saud hawaruhusiwi kumuona Mfalme Salman.

Imearifiwa kuwa, balozi za kigeni, hasa ubalozi wa Marekani mjini Riyadh, unafuatilia kwa karibu hali ya Kiafya ya Salman kwani kuna wasiwasi mkubwa kuwa yamkini mgogoro mkubwa ukaibuka endapo mfalme huyo ataaga dunia.

Mfalme Salman mwenye umri wa miaka 80 anaaminika kuugua ugonjwa wa kupoteza fahamu wa Alzheimer na kwamba ufalme wa Saudia kimsingi unaendeshwa na Mohammad bin Salman. Mashahidi wanasema mfalme huyo wa Saudia huwa anapoteza fahamu mara kwa mara na anaweza kusahau alichokisema dakika chache zilizopita au watu ambao amewajua umri wake wote.

Aidha duru za karibu na ufalme wa Saudia zinadokeza kuwa, mfalme huyo amepata matibabu hospitalini mara kadhaa katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita.

Kutokana na hali hiyo mbaya ya mfalme Salman, imedokezwa kuwa vita vya kuwania uritihi wa kiti hicho vimepamba moto ndani ya ukoo wa Aal Saud. Inasemekana Mfalme Salman amekuwa na mpango wa kumweka kando mrithi wa kwanza wa kiti hicho, Muhammad bin Nayef na badala yake kumrithisha mwanawe kiti hicho.

 

Tags